Friday, June 17, 2016

ENGLAND VS WALES 2-1



TIMU ya taifa ya Uingereza imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza katika michuano ya Ulaya inayoendelea huko Ufaransa baada ya kuifunga Wales kwa mabao 2-1 kwenye mchezo uliomalizika muda mfupi uliopita. Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa Wales ndio waliotangulia kuliona lango la wapinzani wao kwa bao safi la mpira wa adhabu lililofungwa na nyota anayecheza Real Madrid Gareth Bale katika dakika ya 42. Hata hivyo bao hilo halikuwakatisha tama Uingereza na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 56 ambapo nyota wa Leicester City Jamie Vardy alisawazisha bao hilo ingawa ilikuwa inaonekana kama ameotea. Bao la ushindi la Uingereza katika mchezo huo lilifungwa na nyota wa Liverpool Daniel Sturridge katika dakika ya 90 ya mchezo huo. Ushindi huo sasa unaifanya Uingereza kukwea kileleni mwa kundi B wakiwa na alama nne wakifuatiwa na Slovakia na Wales wenye alama tatu kila mmoja huku Urusi ikiburuza mkia kwa kuwa na alama moja. Katika mechi zao za mwisho za makundi Uingereza watacheza Slovakia huku Wales wakipambana na Urusi ambapo timu zote zitakuwa zikijitafuta alama muhimu ili kujihakikishia kusonga mbele katika hatua ya timu 16 bora.

No comments:

Post a Comment