MENEJA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anaamini hamu ya soka aliyonayo Cristiano Ronaldo inamtenganisha na wote akiwa kama mchezaji bora duniani kwasasa. Baada ya kuiongoza Real Madrid kutwaa taji lake la pili la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika kipindi cha miaka mitatu, Ronaldo aliiongoza timu ya taifa ya Ureno kutwaa taji la michuano ya Ulaya kwa kuwafunga wenyeji Ufaransa Juni 10 mwaka huu. Ferguson ambaye alikuwepo Stade de France kushuhudia Ronaldo akitwaa taji hilo la Ulaya, hana shaka kuwa juhudi kubwa alizokuwanazo nyota huyo ndio sababu kubwa ya mafanikio aliyonayo sasa. Ferguson mwenye umri wa miaka 74, ambaye amefanya kazi na Ronaldo kwa miaka sita akiwa na United, amesema uchu na hamu kubwa ya mchezo wa soka aliyonayo Ronaldo ndio inayomfanya kufikia mafanikio hayo hivi sasa. Ferguson aliendelea kudai kuwa Ronaldo amekuwa akijituma kila siku na mara zote amekuwa akitaka kuimarika zaidi na kushinda haswa katika mechi kubwa. Kocha huyo mkongwe amesema kwa kawaida wachezaji wakubwa hucheza kwa kiwango cha juu kwa miaka mitano au sita tu lakini Ronaldo ni tofauti kwa amefanya hivyo kwa zaidi ya miaka 10 ndio anadhani ndio mchezaji bora kabisa kutokea katika kizazi hiki.
No comments:
Post a Comment