KIUNGO wa Chelsea, Oscar amethibitisha kuwa anakaribia kukamilisha usajili wake kwenda klabu ya Shanghai SIPG inayoshiriki Ligi Kuu ya China. Taarifa kutoka nchini Uingereza zimedai nyota huyo wa kimataifa wa Brazil anatarajiwa kujiunga na meneja wake wa zamani Andre Villas-Boas baada ya Chelsea kukubali ofa ya zaidi ya euro milioni 60 kwa ajili ya kiungo huyo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 sasa anatarajiwa kukamilisha usajili wake huo pindi dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Januari mwakani. Akihojiwa Oscar amesema ana uhakika wa asilimia 90 kuondoka Chelsea kwani masuala yalibakia kukamilisha usajili ni kidogo. Oscar amefanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu, Europa League na Kombe la Ligi toka ajiunge na Chelsea akitokea Internacional mwaka 2012. Kama usajili huo ukifanikiwa Oscar atakuwa mchezaji ghali zaidi kusajiliwa katika historia ya Ligi Kuu ya China akimpita Mbrazil mwenzake Hulk ambaye Shanghai ilimsajili kutoka Zenit St Petersburg kwa kitita cha euro milioni 55.8 Juni mwaka huu.

No comments:
Post a Comment