Friday, January 6, 2017

UGANDA WAITOA KIMASOMASO AFRIKA MASHARIKI TUZO ZA AFRIKA.

KIPA wa timu ya taifa ya Uganda, Denis Onyango ameweka historia kwa kuwa kipa wa kwanza kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka anayecheza soka ndani ya Afrika katika sherehe zilizofanyika jijini Abuja, Nigeria jana usiku. Onyango mwenye umri wa miaka 31 alitwaa tuzo hiyo kufuatia kufanya vyema mwaka 2016 akiisaidia klabu yake ya Mamelodi Sundowns kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na timu yake ya taifa ya Uganda. 
Katika tuzo hiyo ya Onyango pia Uganda ilitutoa kimasomaso nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa kuteuliwa kuwa timu bora ya mwaka baada ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39. Kabla ya Onyango tuzo hiyo ilikuwa ikishikiliwa na nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta ambapo aliitwaa wakati akiwa na klabu ya TP Mazembe kabla ya kwenda kucheza Genk ya Ubelgiji kiangazi mwaka jana. Wengine waliotawala tuzo hizo jana ni Riyad Mahrez wa Algeria aliyetwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika akiwashinda Sadio Mane wa Senegal na mshindi wa mwaka jana Pierre-Emerick Aubameyang.

No comments:

Post a Comment