Tuesday, March 7, 2017

IBRAHIMOVIC, MINGS KITANZINI.

MSHAMBULIAJI wa Manchester United Zlatan Ibrahimovic na beki wa Bournemouth Tyrone Mings wamefunguliwa Mashitaka na Chama Soka cha Uingereza-FA kwa kuonyesha mchezo usio wa kiungwana. Wachezaji hao walichezeana faulo mara kwa mara kwenye mechi ya Jumamosi iliyopita ya Ligi Kuu ambapo timu hizo zilitoka Sare 1-1 katika Uwanja wa Old Trafford. Mings alimchezea faulo kwa kumkanyaga kichwani Ibrahimovic aliyekuwa ameanguka chini katika dakika ya 44 na dakika 2 baadae Ibrahimovic alijibu kwa kumpiga kiwiko Mings wakati akipiga kichwa mpira wa kona. Wachezaji hao wamepewa muda hadi kufikia leo kujibu mashitaka yao, FA imeeleza Matukio hayo waliyoshitakiwa nayo hayakuonwa na mwamuzi Kevin Friend lakini yalinaswa kwenye picha za video wakati mchezo ukiendelea. Kwa mujibu wa kanuni za FA, mchezaji kumpiga kiwiko na kumkanyaga mchezaji mwezake kwa makusudi ni faulo ambazo zinastahili kutolewa kadi nyekundu na pia adhabu ya kutocheza mechi tatu.

No comments:

Post a Comment