Sunday, March 4, 2012
WENGER KUMBAKISHA VAN PERSIE EMIRATES.
MENEJA wa Arsenal Arsene Wenger amesema kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa anambakisha mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uholanzi Robin van Persie baada ya kuiwezesha timu hiyo kushinda mabao 2-1 dhidi ya Liverpool katika Uwanja wa Anfield jana. Katika mchezo huo mshambuliaji huyo ndio aliibuka kuwa nyota wa mchezo baada ya kuiwezesha timu hiyo kushinda mchezo huku wakitokea nyuma baada ya kukubali bao la kujifunga mapema katika kipindi cha kwanza. Nahodha huyo wa Arsenal amefikisha mabao 31 katika mashindano yote aliyocheza msimu huu lakini kumekuwa na fununu kuwa mchezaji huyo anaweza kuihama klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu kutokana na mkataba wake kubakia msimu mmoja tu. Lakini Wenger amesema kuwa klabu hiyo itafanya kila iwezalo kuhakikisha inambakisha mshambuliaji huyo kutokana na kiwango bora alichikionyesha msimu huu. Arsenal inakabiliwa na mtihani mzito Jumanne wakati watapokutana na AC Milan katika mchezo wa pili wa hatua ya mtoano wa michuano ya Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya baada ya timu hiyo kukubali kipigo cha 4-0 katika mchezo wa kwanza.
BARCELONA KUKOSA HUDUMA YA SANCHEZ KWA WIKI MBILI.
MSHAMBULIAJI wa pembeni wa timu ya Barcelona atakosekana uwanjani kwa muda wa wiki mbili kufuatia kuumia misuli ya mguu wake wa kulia katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Hispania uliochezwa jana dhidi ya timu ya Sporting Gijon. Nyota huyo wa zamani wa Udinese aliingia uwanjani kipindi cha pili akichukua nafasi ya Cesc Fabregas katika mchezo huo lakini pamoja na ushindi wa timu yake iliyopata wa mabao 3-1 mchezaji huyo aliondoka uwanjani akiwa majeruhi. Timu ya madaktari wa klabu hiyo ilithibitisha kuumia kwa mchezaji huyo majeraha ambayo yatamuweka nje mchezaji huyo kwa muda huo akiwa anapata matibabu. Alexis ambaye aliiwakilisha nchi yake ya Chile wakati ilipocheza na Ghana katikati ya wiki hii ameshaifungia Barcelona mabao 11 toka aliponunuliwa akitokea katika klabu ya Udenese msimu uliopita.
MOURINHO AHOMA KUONGELEA SAFARI YAKE YA UINGEREZA.
MENEJA wa Real Madrid Jose Mourinho amekataa kuongelea mustakabali wake na klabu hiyo huko mbele baada ya kuonekana jijini London katikati ya wiki hii. Kuonekana kwa kocha huyo raia wa Ureno jijini London Jumanne wiki iliyopita kulizua chokochoko kuwa yuko tayari kurejea nchini humo mwishoni mwa msimu huu lakini wakati akihojiwa kabla ya mchezo dhidi ya Espanyol utakaochezwa jioni Mourinho hakutana kuzungumzia lolote kuhusu hilo. Mourinho amesema kuwa kabla ya kwenda huko aliomba ruhusa kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo hivyo hahitaji kufafanua lolote kuhusu maisha yake binafsi kwa mtu mwingine yoyote zaidi ya waajiri wake. Madrid ndio inayoongoza Ligi Kuu nchini Hispania kwa tofauti ya pointi 10 na wapinzani wao wakubwa ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo klabu ya Barcelona.
BRAZIL YAGOMA KUFANYA KAZI NA KATIBU MKUU WA FIFA.
Waziri wa Michezo wa Brazil Aldo Rebelo ametangaza kuwa serikali yake haitaki kushirikiana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke, baada ya malalamiko yake, ambayo amesema hayakubaliki. Kauli hiyo imekuja baada ya Valcke kulalamika juu ya matayarisho ya Brazili ya Kombe la Dunia la mwaka 2014. Rebelo amesema hayo baada ya Valcke kusema kwamba Brazil inaonesha kushughulishwa zaidi na kushinda Kombe la Dunia na kushindwa kuitayarisha nchi hiyo kwa ajili mashindano hayo. Valcke aliendelea kusema kuwa ujenzi wa viwanja vya michezo, miundo mbinu ya usafiri na mahoteli kwa ajili ya washabiki, umezorota hivyo nchi hiyo inahitaji kuzinduka ili kuharakisha shughuli hizo. Rebelo amesema kauli ya Valcke inakera na hailingani na tathmini njema iliyotolewa awali na shirikisho hilo wakati walipokuja kukagua maendeleo ya ujenzi huo. Waziri huyo aliongeza kusema kuwa serikali yake itaendelea kushirikiana na FIFA lakini siyo na Bwana Valcke
Friday, March 2, 2012
TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF.
LIGI KUU VPL YAREJEA TENA
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ambayo iko katika mzunguko wa pili inaendelea tena leo (Machi 2 mwaka huu) na kesho (Machi 3 mwaka huu) baada ya kusimama kwa wiki moja kupisha mechi kati ya timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Msumbiji (Mambas). Leo kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam kutakuwa na mechi kati ya JKT Ruvu na Toto Africans. Mechi za kesho (Machi 3 mwaka huu) ni kati ya Oljoro itakayokuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha. Nayo Polisi Dodoma ikiwa chini ya makocha Rashid Chama na Henry Mkanwa itakuwa ugenini kwenye mashamba ya miwa ya Mtibwa mjini Turiani kuikabili Mtibwa Sugar ya huko. Machi 5 mwaka huu Moro United inayofundishwa na Hassan Banyai itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo iko chini ya Charles Kilinda katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam. Mechi za Machi 7 mwaka huu ni kati ya Oljoro na Toto African (Sheikh Kaluta Amri Abeid), Simba na Kagera Sugar (Uwanja wa Taifa) wakati Azam itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Chamazi.
CHIPUKIZI AINGIA KITUO CHA VIPAJI SENEGAL
Mchezaji Sifael Orgenes Mollel (14) amechaguliwa katika mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream ambao uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwenda kituo cha vipaji (centre of excellence) kilichoko Dakar, Senegal. Mollel kutoka kituo cha Karume alichaguliwa katika mchakato wa mwaka jana uliofanywa na mng’amua vipaji vya soka (scout) kutoka Hispania kwa niaba ya Aspire Football Dreams yenye makao makuu yake Doha, Qatar. Mpango huo wa Aspire Football Dreams kwa Tanzania una vituo 14 na mchakato wa kusaka mchezaji mmoja kila mwaka uhusisha vituo vyote hivyo ambapo kila kimoja kinatakiwa kuwa na watoto wasiopungua 176. Mbali ya Karume, vituo vingine ni Kigamboni, Kawe, Tandika, Makongo, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Morogoro, Bagamoyo mkoani Pwani na Tabata. Mollel atakuwa kwenye kituo hicho cha Dakar kwa muda usiopungua miaka mitatu na anatarajiwa kuondoka nchini Machi 6 mwaka huu. Kwa mwaka wa kwanza wazazi wake watalipwa dola za Marekani 2,500, wa pili dola 2,750 na wa tatu dola 3,000. Mpango wa Aspire Football Dreams ambao unafadhiliwa na mtoto wa Mfalme wa Qatar una vituo viwili vya kuendeleza watoto wenye vipaji (centre of excellence) ambayo viko Doha na Dakar. Lakini mpango huo unaendeshwa katika nchi 16 tofauti duniani. Nchi hizo ni Cameroon, Costa Rica, Gambia, Ghana, Guatemala, Ivory Coast, Kenya, Mali, Nigeria, Paraguay, Rwanda, Senegal, Tanzania, Thailand, Uganda na Vietnam.
U17 KUJINOA KWA RUVU SHOOTING
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) leo (Machi 2 mwaka huu) imeanza kambi yake ya wiki moja ambayo hufanyika kila mwezi jijini Dar es Salaam chini ya kocha Kim Poulsen. Serengeti Boys inayofanya mazoezi Uwanja wa Karume itahitimisha kambi hiyo Machi 9 mwaka huu kwa kucheza mechi na timu ya U20 ya Ruvu Shooting ya mkoani Pwani ambayo iko Ligi Kuu ya Vodacom. Baada ya Serengeti Boys kumaliza kambi Machi 9 mwaka huu, siku hiyo hiyo timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) nayo itaingia kambini chini ya Poulsen katika mpango wa timu hizo kufanya mazoezi ya wiki moja kila mwezi na kucheza mechi moja.
UEFA YASHUSHA BEI YA TIKETI ZA FAINALI cHAMPIONS LEAGUE.
BAADA ya malalamiko mengi kuhusu bei za tiketi za mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la Klabu Bingwa barani Ulaya mwaka uliopita, Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA limeamua kupunguza bei ya baadhi ya tiketi katika fainali ya mwaka huu ambayo inatarajiwa kufanyika May 19 jijini Munich, Ujerumani. Mashabiki wa kawaida wanatarajiwa kulipa kiasi cha euro 70 kwa mwaka huu tofauti na paundi 150 ambayo ndio ilikuwa tiketi ya bei rahisi katika fainali ya mwaka jana kati ya Manchester United na Barcelona katika uwanja wa Wembley, Uingereza. Tiketi ambazo zitakuwa ni ghali zaidi kwa mashabiki wa kawaida mwaka huu zitauzwa kwa euro 370 ambapo mwaka jana mashabiki wa soka walilalamika kutokana na kupanda kwa tiketi hizo kiasi ambacho kilikaribia kufikia ukilinganisha na mwaka 2009. Kwa mwaka huu tiketi zitakuwa chache kutokana na uwanja utakaochezewa mchezo huo wa fainali kumudu kuingia watu 62,500 ukilinganisha na mwaka jana ambapo Wembley ilikuwa na uwezo wa kubeba 86,000. Hiyo inamaanisha mwaka huu kila timu itapata tiketi 17,000 tofauti na mwaka jana ambapo kila timu ilipea tiketi 25,000 huku tiketi ambazo zitabakia watapewa waandaji wa fainali hiyo, vyama 53 vya soka na makampuni ya matangazo.
FIFA KUFUATILIA USHAHIDI WA WARNER JUU YA FEDHA ZA HAITI.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA linafuatilia ushahidi aliowasilisha makamu wa rais wa zamani wa shirikisho hilo Jack Warner kuhusu upotevu wa fedha za msaada za Haiti baada ya tetemeko la ardhi lilitokea nchini humo 2010. FIFA imesema kuwa Warner amewasilisha maelezo yanayoeleza kwa undani kuhusu fedha hizo za msaada kiasi cha dola 250,000 alizoziomba na kupewa kwa ajili ya mradi wa kukuza soka katika nchi za Caribbean. Maofisa wa soka wa Haiti mwezi uliopita wakihojiwa na gazeti moja nchini Uingereza wamesema kuwa wamepokea kiasi cha dola 60,000 pekee kutoka kwa Warner. Wiki iliyopita Shirikisho la Soka la Trinidad na Tobago wamesema kuwa wanapanga kumshitaki Warner ili kuangalia uwezekano kurudisha mamilioni ya dola ambayo yamepotea kinyemela.
Subscribe to:
Posts (Atom)






