Thursday, April 4, 2013

BAADA YA TEVEZ, NASRI NAYE ALAMBWA ADHABU KWA UZEMBE BARABARANI.

KIUNGO wa Manchester United, Samir Nasri amefungiwa kuendesha kwa kipindi miezi sita kwasababu ya kushindwa kulipa faini baada ya kukutwa akiendesha kwa mwendo kasi na gari lake. Adhabu hiyo imekuja baada ya mchezaji mwenzake Carlos Tevez kupewa siku 250 za kuhudumia jamii na pia kufungiwa miezi sita kwakutokuwa na bima. Nasri mwenye umri wa miaka 25 alipigwa faini ya paundi 1,900 lakini alifanikiwa kuiepuka baada ya kuandika barua kuwa hakujua kwamba gari lake aina ya Marcedes lilikuwa limekamatwa na kamera za barabarani kwamba lilizidisha mwendo katika matukio matatu tofauti. Lakini baadae polisi walikata rufani kuhusiana na suala hilo na kumuangushia adhabu hiyo kiungo huyo ingawa bado amepewa nafasi ya kukata rufani kama ataona hakutendewa haki.

OLYMPIQUE MARSEILLE YAOMBA RADHI KWA NIABA YA BARTON.

KLABU ya Olympique Marseille na Joey Barton wameomba radhi kwa mchezaji Thiago Silva na klabu ya Paris Saint-Germain baada ya kiungo huyo wa kimataifa wa Uingereza kumtolea maneno ya kashfa mchezaji huyo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter. Katika taarifa iliyotolewa katika mtandao wa Marseille, klabu hiyo pamoja na kiungo huyo mtukutu walimuomba radhi Silva na klabu yake kwa maneno yasiyokuwa ya kiungwana ambayo yalitumwa na Barton katika twitter. Pia klabu hiyo ilimtaka Barton kumaliza tofauti zilizopo baina yao ambazo zimepelekea mpaka kurushiana na maneno ya kufedhehesha. PSG ilitishia kumchukulia hatua Barton kwa kauli yake ya kudhalilisha aliyotoa kwenda kwa Silva akimfananisha na mwanamke mnene kauli ambayo pia ilingwa vikali na wanaharakati mashoga.

ARSENAL WASABABISHA VURUGU.

KLABU ya Arsenal ya Argentina imejikuta ikipambana na mkono wa sheria baada ya vurugu zilizohusisha maofisa wa polisi wakati wa mchezo wa Kombe la Klabu Bingwa ya Amerika Kusini maarufu kama Copa Libertadores jana. Katika mchezo huo klabu ya Atletico Mineiro ya Brazil ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Arsenal lakini wakati wachezaji wa timu hiyo Argentina wakijaribu kuwafuata waamuzi mara baada ya kipenga cha mwisho walikutana na polisi waliowazuia na kusababisha rabsha kubwa. Mmoja wa maofisa wa polisi aliyejitambulisha kwa jina la Claudia Romaualdo amesema wakati wakijaribu kujipanga ili kuwahakikishia usalama wachezaji wa timu ngeni kwenda kwenye vyumba vyao vya kubadilishia nguo ghafla bila ya kutegemea wachezaji hao walianza kuwashambulia huku mchezaji mmoja akimpiga teke la kifuani. Ofisa huyo amesema lilitokea linasikitisha na sio suala la kimichezo kwani sheria zao zinapovunjwa hawana budi kuchukua hatua zinazostahiki. Wachezaji wanne wa Arsenal wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano baada ya klabu kuzuiwa kuondoka uwanjani mpaka wahusika wa vurugu hizo wapatikane. Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Atletico Mineiro, Eduardo Maluf ameviambia vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa chumba cha kubadilishia nguo walichokuwa wakitumia wachezaji wa Arsenal kimeharibiwa vibaya na wataiomba klabu hiyo kuwalipa gharama ya vitu vilivyoharibiwa.

WENGER AMTETEA WALCOTT.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekanusha madai ya wadau kuwa kiwango cha Theo Walcott kimeporomoka kutokana na kupewa mkataba mpya Januari. Winga huyo wa kimataifa wa Uingereza amekuwa akionyesha kiwango bora katika sehemu ya kwanza ya msimu akifunga mabao 10 katika mechi 18 alizocheza lakini toka akubali kusaini mkataba mpya nyota huyo amefunga bao moja katika mchezo dhidi ya Liverpool miezi miwili iliyopita. Hatahivyo, Wenger amesema haamini kama kushuka kiwango kwa nyota huyo vinahusiana na suala la kupewa mkataba mpya na kuongeza anadhani katika siku za karibuni atarejea katika hali yake ya kawaida. Wenger amesema kama mchezaji huyo angekuwa hajapewa mkataba mpya na kucheza chini ya kiwango watu pia wangesema tofauti hivyo cha muhimu ni mashabiki kumpa muda ili aweze kurejea katika kiwango chake.

ARMSTRONG KUSHIRIKI MASHINDANO YA KUOGELEA.

MWENDESHA baiskeli kutoka Marekani, Lance Armstrong amepanga kurejea katika ulingo wa michezo akiwa kama muogeleaji. Armstrong mwenye umri wa miaka 41 ambaye alikumbwa na kashfa ya kutumia dawa za kuongeza nguvu na kunyang’anywa mataji yake yote saba ya mbio za baiskeli za Tour de France, alijiandikisha kushiriki mashindano ya kuogelea yatakayofanyika jijini Texas mwishoni mwa wiki hii. Wakala wa kupambana na dawa za kuongeza nguvu nchini Marekani-Usada, ambao mbali na kumvua mataji yake lakini pia walimfungia maisha kushiriki michuano yoyote ya baiskeli. Januari mwaka huu Armstrong alikiri kutumia dawa za kuongeza nguvu katika mataji yake yote saba ya Tour de France aliyonyakuwa katika kipindi cha mwaka 1999 mpaka 2005 katika mahojiano ya luninga na mtangazaji maarufu Oprah Winfrey.

Wednesday, April 3, 2013

IYA MOHAMMED AZUIWA KUSAFIRI NJE YA CAMEROON.

VYOMBO vya habari nchini Cameroon vimeripoti kuwa polisi katika Uwanja wa Ndege wa Douala wamezuia pasi ya kusafiria ya rais wa Shirikisho la Soka nchini humo Iya Mohammed ambaye alikuwa akisafiri kuelekea nchini Ufaransa. Mohammed ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya umma ya katani-Sodecoton ameema likuwa akitaka kusafiri kuelekea jijini Paris, Ufaransa kwa ajili ya mkutano na alikuwa amekamilisha taratibu zote za safari wakati polisi wawili walipotokea na kudai wametumwa kumzuia asisafiri kwenda na kunyang’anya pasi yake. Amesema hakuna sababu yoyote aliyopewa kuhusiana na tukio hilo kwake zaidi ya kuchukua pasi yake na kuondoka nayo. Baraza la udhibiti wa bajeti na fedha, ambalo lilisimamia Sodecoton lilitoa taarifa Machi 29 mwaka huu wakimtuhumu Mohammed kwa matumizi mabaya ya ofisi ambayo yalipelekea kampuni hiyo kupata hasara ya dola milioni 18. 

KROOS NJE MSIMU MZIMA.

Klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani inatarajia kukosa huduma ya kiungo wake wa kati Toni Kroos kwa msimu mzima uliobakia baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani kuumia kinena katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus. Kroos mwenye umri wa miaka 23 alipata maumivu hayo katika mguu wa kushoto katika dakika ya 13 ya mchezo huo ambao Bayern ilishinda kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Alianz Arena. Daktari wa Bayern, Hans-Wilhelm Mueller Wohlfahrt amesema kuwa Kroos atakaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki sita mpaka nane kutokana na ukubwa wa tatizo lililompata. Bayern ambayo inafukuzia kuwa timu ya kwanza nchini Ujerumani kushinda mataji yote matatu kwasasa wako kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo kwa tofauti ya alama 20 na kuna uwezekano wa kunyakuwa Kombe la Ligi kama wataifunga Eintracht Frankfurt katika mchezo wa fainali Jumamosi.