MWANARIADHA nyota wa mbio fupi, Usain Bolt amedhamiria kutobweteka kutokana na kukosekana kwa mahasimu wake wakati atakapojaribu kurejesha tena taji la mbio za mita 100 alilopoteza miaka miwili iliyopita. Bolt ambaye alitetea medali zake za olimpiki mwaka uliopita, amesema baada ya kutua jijini Moscow kwa ajili ya mashindano ya raiadha ya dunia kuwa haogopeshwi na kilichotokea jijini Daegu mwaka 2011 wakati alipoenguliwa kwa kuanza kukimbia kabla ya wenzake. Zikiwa zimebakia siku sita kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, Bolt amesema madhumuni makubwa yam bio za mita 100 za mwaka huu atazoshiriki ni kuhakikisha anarejesha taji lake na kwa maandalizi aliyopata hana shaka katika hilo. Mahasimu wa Bolt wa karibu katika mbio hizo Tyson Gay wa Marekani na Asafa Powell wa Jamaica hawatashiriki baada ya kushindwa vipimo vya dawa zilizopigwa marufuku wakati mjamaica mwingine Yohane Blake atashindwa kutetea taji hilo kwasababu ya majeraha.
Monday, August 5, 2013
NEYMAR ASUMBULIWA NA TATIZO LA UPUNGUFU WA DAMU.
MKURUGENZI wa michezo wa klabu ya Barcelona, Andoni Zubizarreta amedai kuwa pamoja na mshambuliaji wao nyota Neymar kusumbuliwa na tatizo la upungufu wa damu kwao sio suala linalowatia mashaka kwa sasa. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ambaye alijiunga na Barcelona akitokea Santos kwa ada ya euro milioni 57 katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi, aligundulika kuwa na tatizo hilo la upungufu wa damu ambalo linahisiwa kusababishwa na vipimo vingi vya damu alivyofanya katika siku za karibuni. Lakini Zubizarreta alisisitiza kuwa hali hiyo ya Neymar mwenye umri wa miaka 21 ni kitu ambacho madaktari wa klabu wanaweza kukimaliza na sio cha kuleta wasiwasi sana kuhusu kiwango chake. Zubizarreta amesema watajaribu kumsaidia ili kuhakikisha anakuwa katika afya njema kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi a,bapo Barcelona wataanza kutetea taji lao kwa kuchuana na Levante katika Uwanja wa Camp Nou Agosti 18 mwaka huu.
DROGBA AENDELEA KUINYANYASA ARSENAL.
MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ivory Coast na timu ya Galatasaray ya Uturuki, Didier Drogba ameendelea kuinyanyasa klabu ya Arsenal baada ya kuifungia klabu yake mabao yote mawili kwenye ushindi wa 2-1 katika Kombe la Emirates jana. Drogba alikuwa amejenga tabia ya kuifunga Arsenal kila wanapokutana nayo wakati akiwa Chelsea na aliendeleza wimbi hilo jana baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba katika kipindi cha pili kwa kuisawazishia na kuifungia bao la ushindi timu yake katika fainali michuano hiyo inayoshirikisha timu nne. Kikosi cha Arsenal kinachonolewa na Arsene Wenger inatabidi kijilaumu chenyewe kwa kushindwa kutumia nafasi walizokuwa wamepata na ukosefu huo wa umakini kwenye umaliziaji ndio unaosababisha kocha huyo kupambana kujaribu kumuongeza Luis Suarez ili kuimarisha safu ya ushambuliaji. Wenger mpaka sasa amefanya usajili mmoja pekee wa mshambuliaji kinda Yaya Sanogo mwenye umri wa miaka 20 kutoka klabu ya AJ Auxerre ya Ufaransa.
Saturday, August 3, 2013
BOLT APANGA KUREJESHA UBINGWA WAKE WA MBIO ZA MITA 100 ALIOPOTEZA JIJINI DAEGU MWAKA 2011.
MWANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt amepanga kuibuka na ushindi katika mashindano ya dunia ya mbio za mita 100 baada ya kupoteza medali hiyo mwaka 2011 jijini Daegu. Bolt ambaye ni bingwa mara sita wa medali za dhahabu katika michuano olimpiki, alienguliwa katika mashindano ya jijini Daegu kwa kuanza kukimbia kabla ya kuruhusiwa hatua ambayo ilipelekea Mjamaica mwenzake Yohane Blake kushinda mbio hizo baada ya kurudiwa. Toka wakati huo Bolt anaonekana kusahau kipindi hicho kigumu na kuingia jijini Moscow akiwa mwanariadha anayepewa nafasi kubwa ya kushinda baada ya Blake kujitoa kutokana na majeruhi na wengine kama Tyson Gay wa Marekani na Asafa Powell wa Jaimaica wao wakijitoa baada ya kushindwa vipimo vya dawa za kuongeza nguvu. Akihojiwa mara baada ya kushinda mbio za mita 100 za Diamond League zilizofanyika jijini London wiki iliyopita, Bolt amesema kocha wake amekuwa akimkumbusha juu ya tatizo lake kwenye kuanza lakini akamtaka kuacha kukumbuka yaliyotokea nyuma.
ISHA JOHANSEN RAIS MPYA WA SHIRIKISHO LA SOKA SIERRA LEONE.
PAMOJA na utata unaoendelea, Isha Johansen amethibitishwa kuwa rais mpya wa Shirikisho la Soka nchini Sierra Leone kutokana na kupita bila kupigwa katika uchaguzi baada ya wagombea wengine kuenguliwa katika kinyang’anyiro hicho kwa kukosa vigezo. Isha mwenye umri wa miaka 48 anakuwa mwanamke wa pili kuwa kiongozi katika ulimwengu wa soka pamoja na Lydia Nsekera ambaye ni rais wa Shirikisho la Soka nchini Burundi. Kazi ya kwanza Johansen akiwa madarakani ni kuhakikisha ligi ya soka ya nchi hiyo inaendelea baada ya vilabu kugomea kutokana na wagombea watatu wa nafasi hiyo kufungiwa. Uchaguzi wa Sierra Leone umekuwa ukikumbwa na utata kwa karibu mwaka mzima sasa na bado umeendelea kuzua mjadala juu ya wajumbe wenye haki ya kupiga kura katika uchaguzi ambao Johansen ameshinda.
BALE KUIKOSA MONACO KUTOKANA NA MAJERUHI.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Gareth Bale anatarajiwa kukosa mchezo wa kirafiki kati ya timu yake na Monaco ya Ufaransa kutokana na majeruhi yanayomsumbua. Kwa mujibu wa mtandao wa The Sun mshambuliaji wa kimataifa wa Wales aliagana na wachezaji wenzake jijini London mapema Ijumaa kabla ya hawajapaa kuelekea jijini Monte Carlo kwa ajili ya mchezo huo wa kirafiki. Mbali na kuukosa mchezo huo Bale pia anatarajiwa kuukosa mchezo wa kirafiki wa timu yake ya taifa ya Wales dhidi ya Ireland unaotarajiw akupigwa jijini Cardiff Agosti 14 mwaka huu. Wakati Bale akipambana kurejea katika hali yake ya kawaida, mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy anatarajiwa kukaa chini kwa mara ya kwanza kuzungumza na rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez jijini Miami wiki ijayo kwa ajili ya mazungumzo juu ya uhamisho wa mchezaji huyo. Kama mazungumzo hayo yakienda vizuri, Bale mwenye umri wa miaka 24 anatarajiwa kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi, heshima ambayo kwasasa inashikiliwa na Cristiano Ronaldo ambaye alihama kutoka Manchester United kwenda Madrid kwa ada ya paundi milioni 80 mwaka 2009.
GERRARD AMTAKA SUAREZ KUBAKIA LIVERPOOL.
KIUNGO mahiri wa klabu ya Liverpool, Steven Gerrard amemtaka Luis Suarez kubakia klabuni hapo ikiwa ni mwaka mmoja umepita toka Gerrard mwenyewe kukataa kuondoka kwenda kwenye timu inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akiongea kabla ya mchezo dhidi ya Olimpiacos katika Uwanja wa Anfield, Gerrard alibainisha kuwa alikuwa na nafasi ya kujiunga na klabu inayoshiriki michuano ya Ulaya msimu uliopita na kumsisitizia Suarez hatakiwi kufanya maamuzi ya haraka kuondoka Liverpool. Gerrard amesema mshambulijai huyo nyota wa Uruguay mwenye umri wa miaka 26 hatakiwi kuwa na haraka kwani ofa kubwa zaidi zitamiminika kwa ajili yake kama akiendelea kubakia Liverpool kwa msimu mwingine mmoja. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 aliendelea kudai kuwa Suarez anastahili kucheza katika moja vilabu vikubwa kabisa kama Real Madrid au Barcelona hivyo akisubiri hakuna shaka kwamba watamuita katika kipindi kifupi kijacho.
Subscribe to:
Posts (Atom)






