Thursday, January 1, 2015

HERI YA MWAKA MPYA WA 2015.

MPENZI MSOMAJI WA BEKI3 TUNASHUKURU KWA KUWA PAMOJA NASI KWA KIPINDI CHOTE CHA MWAKA 2014 TUKIJUZANA HAYA NA YALE YALIYOTOKEA KATIKA ULIMWENGU WA MICHEZO HUSUSANI SOKA NDANI NA NJE, TUNAPENDA KUKUAHIDI KUWA MWAKA HUU MPYA WA 2015 TUTAENDELEA KUWA PAMOJA NA NAWE NA KUENDELEA KUPASHANA ZAIDI YA ILIVYOKUWA MWAKA ULIOPITA HIVYO ENDELEA KUWA NASI, ASANTE.

TETESI ZA USAJILI: MESSI AMTAKA LAVEZZI, MOURINHO KUMFUATA REUS DORTMUND.

WAKATI dirisha dogo la usajili likiwa limefunguliwa rasmi leo kumekuwa na taarifa na tetesi mbalimbali za usajili zinazoendelea kila pembe barani Ulaya. Tukianzia nchini Hispania kumekuwa taarifa zinazodai kuwa mshambuliaji nyota wa Barcelona Lionel Messi ameiomba timu hiyo kumsajili Ezequiel Lavezzi kutoka klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa. Taarifa hizo zimeendelea kudai kuwa Messi anataka kucheza pamoja na mshambuliaji mwenzake huyo kutoka Argentina. Tukisogea nchini Uingereza nako kuna tetesi kuwa meneja wa Chelsea Jose Mourinho amemuomba bosi wake Roman Abromovic kumsajili nyota wa kimataifa wa Ujerumani Marco Reus kutoka klabu ya Borussia Dortmund. Tukibakia hukohuko Uingereza, Arsenal nao wameibuka baada ya kudaiwa kuwa wanamuwinda kuingo wa Atletico Madrid Mario Suarez wakati kocha wa timu hiyo Arsene Wenger akijaribu kuimarisha kikosi chake. Tukirejea nchini Hispania kuna taarifa kuwa kampuni ya vifaa vya michezo kutoka Marekani ya Ander Armour inadaiwa kuanza mazungumzo na klabu ya Barcelona kwa ajili ya udhamini wa jezi zao hivyo kuzusha tetesi kuwa mkataba baina yake na kampuni ya Nike unaweza kusitishwa wakati wowote.

BORO YAKUBALIANA NA CHELSEA KUENDELEA KUMTUMIA BAMFORD.

KLABU ya Middlesbrough imethibitisha kuongeza makubaliano ya mkopo na klabu ya Chelsea kwa ajili ya mshambuliaji Patrick Bamford mpaka mwishoni mwa msimu huu. Bamford amekuwa akionyesha kiwango kizuri toka ajiunge na Boro kwa mkopo wakati wa majira ya kiangazi mwaka jana akifunga mabao nane katika mechi 19 alizoichezea timu hiyo ambayo inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza. Mkataba wake wa awali ulikuwa umalizike januari hii lakini Middlebrough wameamua kuongeza mkopo wa mshambuliaji mwenye umri wa miaka 21 ili aweze kuwasaidia katika kampeni zao za kurejea Ligi Kuu. Meneja wa timu hiyo Aitor Karanka amedai kuwa bamford anafurahia kuwepo hapo kwani anajifunza na kuimarika jambo ambalo ni muhimu kwa malengo yake pamoja na klabu. Bamford tayari ameshacheza kwa mkopo katika klabu za MK Dons na Derby County toka asajiliwe na Chelsea akitokea Nottingham Forest januari mwaka 2012.

CITY YAMUONGEZA MKATABA LAMPARD.

KLABU ya Manchester City imemuongeza mkataba kiungo Frank Lampard ambao utamalizika mwishoni mwa msimu huu. Mkataba wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 36 kutoka klabu ya New York City ulimalizika jana lakini sasa ataendelea kuwemo mpaka majira ya kiangazi na kumfanya kukosa mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu nchini Marekani-MLS. Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Uingereza amefunga mabao sita katika mechi 17 alizoichezea City msimu huu. Lampard alisajiliwa na New York baada ya kuachwa na Chelsea Juni mwaka huu ambapo muda wake rasmi wa kuanza kucheza soka utathibitishwa baadae kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo.

ANCELOTTI ATAMBA MADRID KUTETEA TAJI LAKE LA ULAYA.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti ametamba kuwa timu yake inaweza kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu huku akidai kikosi ni imara duniani kwasasa. Madrid waliharibiwa utawala wao kwa mwaka 2014 kwa kichapo cha mabao 4-2 walichopata kutoka kwa AC Milan katika mchezo wa kirafiki lakini matokeo hayo hayawezi kufuta mambo mengi mazuri yaliyofanyw ana timu hiyo kwa mwaka jana. Ushindi waliopata dhidi ya San Lorenzo ya Argentina katika mchezo wa fainali ya Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya uliwaongezea mataji na kuongeza idadi ya mechi za kimashindano walizoshinda kufikia 22. Ancelotti ana uhakika kuwa mafanikio zaidi yanategemewa kupatikana katika mwaka huu kutokana na kikosi imara walichonacho. Kocha huyo amesema mwaka huu wanataka kushindana katika kila shindano na kutokana na uimara wa kikosi chao ana uhakika watatoa changamoto ya kutosha kwa wapinzani wao watakaokutana nao.

MMILIKI WA WIGAN AFUNGIWA KWA UBAGUZI.

MMILIKI wa klabu ya Wigan Athletic Dave Whelan amefungiwa kwa wiki sita kujishughulisha na masuala yeyote ya michezo na kutozwa faini ya paundi 50,000 kwa kutoa kauli ya kibaguzi kuwalenga watu wenye asili ya Uyahudi na Wachina. Tajiri huyo mwenye umri wa miaka 78 ambaye amepewa wiki moja kukata rufani kuhusiana na adhabu hiyo pia ametakiwa kuhudhuria darasa la ushauri litakalokuwa likiendeshwa na Chama cha Soka cha Uingereza. Mwezi uliopita Whelan alikubali tuhuma hizo lakini alikataa kauli alizotoa wakati akihojiwa na gazeti moja kuwa za kibaguzi. Novemba mwaka huu Whelan alidai kuwa atajiuzulu kama akikutwa na hatia ya kuwa mbaguzi.

SWANSEA YAKUBALI ADHABU YA SHELVEY.

KLABU ya Swansea City imekubali adhabu ya kiungo Jonjo Shelvey kufungiwa mechi nne baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Liverpool Emre Can. Shelvey alimtwanga kiwiko Can usoni wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ambao Swansea walitandikwa mabao 4-1 na Liverpool. Katika mchezo huo mwamuzi Andre Marriner hakuliona tukio hilo hivyo alimruhusu Shelvey mwenye umri wa miaka 22 kuendelea na mchezo. Katika taarifa yake iliyotumwa katika mtandao Swansea walithibitisha kukubali adhabu hiyo huku Chama cha Soka cha Uingereza-FA kikidai kuwa pamoja na kuwa tukio hilo halikuonwa na mwamuzi lakini picha za video ndio zilizothibitisha kutokea kwake.