Sunday, August 21, 2011

AZAM YAANZA LIGI VYEMA.


DAR ES SALAAM, Tanzania
BAO pekee la mshambuliaji John Bocco wa Azam FC katika dakika ya 45  limepelekea timu hiyo kuanza vyema mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom VPL kwa kuifunga Moro United 1-0 mchezo uliochezwa leo katika uwanja wa Azam Stadium, Chamazi, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni moja kati ya michezo mitano iliyochezwa leo katika ufunguzi wa mechi za ligi kuu kwa msimu huu wa mwaka 2011/2012, Azam FC wameanza vema kwa kuchukua pointi tatu muhimu.

Mchezo wa leo haukuwa mzuri kwa timu zote labda ni kutokana na uoga, timu zote zilicheza kwa kutegeana na kupeleka mashambulizi langoni kwa mwenzake huku kila mchezaji akitafuta nafasi ya kufunga lakini mbinu za kupanga mashambulizi haikuwa murua.

Azam FC walipata goli hilo pekee katika mchezo huo kwa mkwaju wa penati iliyoamuliwa na mwamuzi wa David Paul baada ya walinzi wa Moro United kumwangusha mshambuliaji John Bocco wa Azam FC.

Bocco alipiga penati hiyo iliyomshinda mlinda mlango wa Moro, Lucheke Mussa na kuandika goli kwa Azam FC, goli ambalo lilidumu hadi kumalizika kwa mchezo huo.

Mchezaji Kipre Tchetche kama kawaida yake alisumbua lango la Moro lakini haikuwa bahati yake, huku Ramadhani Chombo alikosa nafasi mbili za wazi kipindi cha kwanza, upande wa Moro mshambuliaji mwenye mwili mkubwa Gaudence Mwaikimbi alikuwa tishio kwa mabeki wa Azam FC ambapo shambulizi lake la dakika ya 27 lililogonga mwamba.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko kuimarisha vikosi vyake Moro waliwatoa Sultani Kasikasi na George Mkoba nafasi zao kuchukuliwa na Jerome Lambele na Bakari Mpakala, Azam FC walifanya mabadiliko kwa kuwarudisha benchi Ibrahim Mwaipopo na Kipre Tcheche na kuwapa nafasi Salum Aboubakar na Khamis Mcha mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya mchezo lakini hayakubadili matokeo.

Katika michezo mingine Toto Africa wameifunga Villa Squad 3-0, African Lyon imetoka suluhu na Police Dodoma huku Kagera Sugar waliocheza na Ruvu Shooting na Coastal Union walicheza na Mtibwa Sugar zote zimetoka sare ya 1-1.

Kikosi cha Azam FC kilichofungua pazia la ligi kuu: Obren Cirkovic, Agrey Moris, Erasto Nyoni, Waziri Ally, Said Morad, Mwaipopo/Salum Aboubakar, Abdulhalim Humud,Mrisho Ngassa, John Bocco, Kipre Tchetche/Mcha na Ramadhan Chombo Redondo.

Moro Utd, Lucheka Mussa, Tumba Swed, George Mkoba, Gideon Sepo, Godfrey Wambura, Rajab Zahir, Benedict Ngassa, Salum Telela, Mwaikimba na Sultan Kasikasi.

MATOKEO MENGINE YA MICHEZO ILIYOCHEZWA JANA NI KAMA IFUATAVYO.

COASTAL UNION 1:1 MTIBWA SUGAR

TOTO AFRICANS 3: 0 VILLA SQUARD

POLISI 0: 0 AFRICAN LYON




No comments:

Post a Comment