Monday, August 15, 2011

KUZIONA SIMBA NA YANGA NGAO YA JAMII SHS. 5,000, TFF YAMKOMALIA KAGO.


Angetile Osiah, Katibu Mkuu TFF.

DAR ES SALAAM, Tanzania
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa Ngao ya Jamii (Community Shield) utakaowakutanisha watani wa jadi Simba na Yanga Agosti 17 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema maandalizi yote kwa ajili ya mchezo huo ambao umedhaminiwa na Kampuni ya Mafuta ya Big Bon tayari yamekamilika.

Alisema katika mchezo huo viingilio vya juu kabisa yaani VIP A kitakuwa ni shilingi 50,000 wakati kiingilio cha chini kabisa jukwaa la viti vya bluu (Blue Stand) kitakuwa shilingi 5,000, viingilio vingine katika mchezo huo vitakuwa ni VIP B shs. 25,000, VIP C shs. 20,000, viti vya rangi ya chungwa mzunguko (Orange Curve) shs. 10,000 na viti vya rangi ya kijani (Green Stand) shs. 7,000.

Alisema ulinzi kwa ajili ya mchezo huo ambao utachezwa majira ya saa mbili za usiku utakuwepo ndani na nje ya uwanja katika kipindi chote cha mchezo na baada ya mchezo hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kushuhudia mchezo huo pasipo hofu yoyote.

Wakati huohuo TFF imesema inasikitishwa na tuhuma anazotupiwa Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo Sadi Kawemba kwamba ndiye aliyemzuia mchezaji Kago wa Simba asipitishwe kuichezea timu hiyo katika mechi hiyo ya ngao ya jamii.

Angetile alisema mkataba Simba waliompa mchezaji huyo unaonyesha kuwa mchezaji huyo ni wa kulipwa tofauti na barua walioiwasilisha TFF kuwa wamemsajili mchezaji huyo kama wa ridhaa.

Alisema walichotakiwa kufanya kuja kwao (TFF) ili wapewe maelekezo na taratibu za kufuata na kufanya kama walivyofanya kutoka tuhuma ambazo hazina msingi wowote.

No comments:

Post a Comment