Boniface Wambura, Ofisa Habari wa TFF. |
DAR ES SALAAM, Tanzania
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limetangaza kuwa mchezo wa Ngao ya Jamii (Community Shield) kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Mabingwa watetezi Yanga na Simba utachezwa Agosti 17 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa mbili za usiku.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mchezo huo umewekwa muda huo kutokana na sababu kubwa mbili mojawapo ikiwa ni kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kingine ni kuwa siku hiyo ya Agosti 17 ni siku ya kazi.
Alisema pambano hilo litatanguliwa na mechi ya vikosi vya pili vya timu hizo mbili (U20) Simba B na Yanga B ambayo itaanza saa kumi za jioni.
Alisema mchezo wa Ngao ya Jamii baada ya dakika 90 kama mshindi hatapatikana, zitaongezwa dakika 30. Katika muda huo nao kama mshindi atakuwa bado hajapatikana, itatumika mikwaju ya penalti.
Alisema mechi hiyo imepata mwekezaji (Bigbon) na hivi sasa wadau wake wakuu- Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu husika ziko katika mazungumzo ya mwisho mwekezaji huyo. Kwa redio ambazo zinataka kutangaza mechi hiyo moja kwa moja zinatakiwa kuwasiliana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF ili kupewa masharti ya kufanya hivyo.
Pia unafanyika utaratibu wa kuuzwa futari uwanjani mara baada ya mechi ya vikosi vya pili ili kuwawezesha washabiki waliofunga kutohangaika kutafuta sehemu ya kufuturu.
No comments:
Post a Comment