Saturday, August 20, 2011

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF.


MSIMU MPYA LIGI KUU YA VODACOM
Msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom 2011/2012 unaanza kesho (Agosti 20 mwaka huu) ambapo timu 10 kati ya 14 zinazoshiriki katika ligi hiyo zitakuwa viwanjani. Mechi za kesho ni Coastal Union v Mtibwa Sugar (Mkwakwani, Tanga), Kagera Sugar v Ruvu Shooting (Kaitaba, Bukoba), Toto Africans v Villa Squad (Kirumba, Mwanza) na Polisi Dodoma v African Lyon (Jamhuri, Dodoma).

Mechi nyingine ni Azam v Moro United itakayochezwa Chamazi, Dar es Salaam wakati mechi za Jumapili (Agosti 21 mwaka huu) ni Oljoro JKT v Simba (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), na Yanga watakaokuwa wenyeji wa JKT Ruvu.

WAAMUZI WA KATI
Waamuzi wa kati (centre referees) 16 wameteuliwa kuchezesha Ligi Kuu. Waamuzi hao ni Ronald Swai (Arusha), Isihaka Shirikisho (Tanga), Peter Mujaya (Mwanza), Amon Paul (Mara), Mathew Akrama (Mwanza), Ibrahim Kidiwa (Tanga), Dominic Nyamisana (Dodoma), David Paul (Mtwara), Hashim Abdallah (Dar), Martin Saanya (Morogoro), Orden Mbaga (Dar), Kennedy Mapunda (Dar), Israel Mujuni (Dar), Alex Mahagi (Mwanza), Abdallah Kambuzi (Shinyanga) na Thomas Mkombozi (Kilimanjaro).

Pia wameteuliwa waamuzi wa akiba (reserve referees) sita ambao watatumika wakati wowote watakapohitajika. Waamuzi wasaidizi (assistant referees) walioteuliwa kuchezesha ligi ni 34. Kwa upande wa waamuzi wasaidizi wa akiba walioteuliwa ni kumi. Hivyo jumla ya waamuzi watakaotumika kwenye ligi hiyo ni 50.

MAKAMISHNA WA MECHI
Jumla ya makamishna (match commissioners) 24 wameteuliwa kusimamia mechi za ligi hiyo. Kati ya hao 20 ni wa zamani na wanne ni wapya. Makamishna wapya ni Charles Ndagala, Victor Mwandike, Godbless Kimaro na Hamis Tika.

Makamishna wa msimu uliopita walioteuliwa tena ni Hamis Kissiwa, David Lugenge, Abdallah Mitole, Charles Komba, George Komba, Jimmy Lengwe, Amri Kiula, James Mhagama, Fulgence Novatus, Pius Mashera, Michael Bundara, Gabriel Gunda, Mohamed Nyange, Mwijage Rugakingira, Arthur Mambeta, Paul Opiyo, Edward Hiza, Salim Singano, William Chibura na Omary Mwamela.

Uteuzi wa makamishna kama ilivyo kwa waamuzi ulifanyika baada ya kuhudhuria kozi na kufanya mitihani. Kwa upande wa makamishna ambao hawakufanya vizuri, watalazimika kurudia mitihani kabla ya kuteuliwa tena.

NAULI KWA TIMU ZINAZOSHIRIKI LIGI
Kila timu inayoshiriki ligi itapata jumla ya sh. milioni 26.3. Fedha hizo zitatolewa kwa awamu tano tofauti kuanzia mwezi huu. Agosti kila timu itapata sh. 4,732,142, Septemba (sh. 4,732,142), Oktoba (sh. 5,622,321), Januari (sh. 5,622,321) na Machi (sh. 5,622,321).

Jumla ya fedha kutoka kwa mdhamini wa ligi, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ambazo zitatumika kwa ajili ya nauli kwa timu zote katika msimu mzima ni sh. 368,637,458.

MECHI YA STARS, ALGERIA
Tumeiandikia barua Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuomba iruhusu mechi ya mchujo ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani Equatorial Guinea na Gabon kati ya Taifa Stars na Algeria (Desert Warriors) ichezwe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ombi letu limetokana na ukweli kuwa tulishaliarifu Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) miezi mitatu iliyopita kuwa mechi hiyo itachezwa katika uwanja huo. Taarifa hiyo pia tuliipa Algeria ambayo imeshatuma ujumbe wake kukagua hoteli ambayo timu yao itafikia.

Kwa upande wa CAF uamuzi wa kubadili uwanja hivi sasa maana yake kuwa itatupiga faini, lakini vilevile TFF tutalazimika kuingia gharama za kusafirisha kwa ndege timu zote mbili pamoja na waamuzi kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo.

No comments:

Post a Comment