Wachezaji wa Esperance wakishangilia bao pekee katika mchezo huo dhidi ya Al Hilal ya Sudan mchezo ulichezwa Jumapili. |
TIMU ya Esperance ya Tunisia wamejiweka katika nafasi nzuri ya kutinga fainali ya michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika kwa pili mfululizo baada ya kuifunga kwao Al Hilal ya Sudan kwa bao 1-0 Jumapili.
Mchezo wa marudiano baina ya timu hizo unatarajiwa kuchezwa katikati ya mwezi Octoba jijini Tunis na matokeo yoyote ya sare yataivusha katika hatua ya fainali Esperance, ambao bado wanauguza kidonda cha kufungwa jumla ya mabao 6-1 katika hatua ya fainali dhidi ya TP Mazembe ya DRC msimu uliopita.
Kiungo wa pembeni wa esperance Youssef Msakni ndio aliyefunga bao hilo pekee katika Uwanja wa Al Hilal, Omdurman dakika ya nne baada ya mpira kuanza.
Hilo ni bao la nne kwa Msakni (20) katika mashindano hayo msimu huu, lakini ni la kwanza toka alipoifungia timu yake hiyo bao mwezi Aprili wakati alipochangia bao moja katika ushindi wa mabao 5-0 uliyopata timu yake dhidi ya timu ya Senegal ya Diaraf Dakar.
Kwa kawaida Al Hilal ni wazuri zaidi wakiwa nyumbani kuliko ugenini hivyo watakuwa na wakati mgumu kuvuka hatua hiyo ya nusu fainali kwa mara ya tatu ndani ya miaka mitano.
Wydad Casablanca ya Morocco ikiwa nyumbani ilishinda bao 1-0 dhidi ya Enyimba ya Nigeria katika mchezo mwingine wa nusu fainali ya michuano hiyo uliochezwa Jumamosi, bao ambalo lilifungwa na Pascal Angan kwa mpira wa adhabu dakika moja kabla ya kulia kwa kipenga cha mwisho.
Fainali za michuano hiyo zinatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Novemba mwaka huu ambapo kati ya Wydad au Enyimba ndio watakuwa wenyeji katika mchezo wa kwanza kushindania zawadi ya dola milioni 1.5 (bilioni 17) pamoja na tiketi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa ya dunia itakayofanyika Japan, mwishoni mwa mwaka huu.
No comments:
Post a Comment