KOCHA wa timu ya Taifa "Taifa Stars" Jan Poulsen amesema tofauti ya ubora wa viwango ndio chanzo kikubwa cha timu hiyo kufanya vibaya katika mchezo wake dhidi ya Morocco.
Poulsen alizungumza hayo leo asubuhi wakati kikosi cha Stars kilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, kwa ndege ya Shirika la Ndege Qatar.
Amesema timu hiyo ilionyesha kiwango kizuri katika mchezo huo ndio maana mpaka wanakwenda mapumziko walikuwa wako nguvu sawa kwa kufungana bao 1-1, kabla ya kipindi cha pili ambapo tulizidiwa mbinu kidogo na kujikuta tukifungwa bao la pili kabla ya kumalizia la tatu dakika za lala salama.
"Wakati mwingine mashabiki wa soka hapa nchini wanasahau kuwa timu yetu "Stars" iko katika nafasi ya ngapi kwa ubora wana viwango vya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) ukilinganisha na Morocco tuliocheza nao." alisema Poulsen wakati akihojiwa na waandishi wa habari uwanjani hapo.
Amesema kwasasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo dhidi ya Chad ili waweze kufanikiwa kuingia katika hatua ya makundi kwa michezo yakutafuta tiketi ya kucheza Kombe la Dunia litalofanyika nchini Brazil 2014.
Stars inabidi ipigane kufa na kupona kushinda mchezo dhidi ya Chad ili kupata nafasi hiyo, kwani wakishindwa mchezo huo timu hiyo itakosa nafasi kama hiyo kwa muda wa miaka miwili, na kama wakifanikiwa basi itajiunga timu zingine katika kundi C ambazo ni Gambia, Morocco na Ivory Coast ambazo zenyewe zilipita moja kwa moja kwa viwango vizuri katika orodha ya FIFA.
No comments:
Post a Comment