Sunday, November 27, 2011

CECAFA CHALLENGE CUP: HARAMBEE STARS KUIKWAA MALAWI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Kenya-Harambee stars Francis Kamanzi amesema kikosi kitakuwa kikishambulia zaidi wakati kitakapocheza na Malawi katika michuano ya Kombe la Challenge utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo mchana. Kikosi hicho kiliwasili jana mchana tayari kwa mashindano hayo huku kikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuitoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 7-0 katika mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Dunia 2014. Kocha huyo amesema Malawi ni timu nzuri hivyo hawawezi kuwadharau lakini akatamba kuwa kikosi chake imara huku akisifu washambuliaji wake wenye kasi kuwa watasaidia kuibuka na ushindi katika mchezo huo. Harambee Stars imepangwa katika kundi C wakiwa na timu za Sudan, Malawi na Ethiopia katika michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA.

No comments:

Post a Comment