CECAFA CHALLENGE CUP: ZIMBABWE YACHUKUA NAFASI YA NAMIBIA.
Nicholaus Musonye, Katibu Mkuu CECAFA
Zimbabwe itachukua nafasi ya Namibia kwenye michuano ya Cecafa inayoanza Ijumaa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Namibia iliyokuwa imepangwa Kundi A pamoja na wenyeji Tanzania, Rwanda na Djibouti imejitoa kwa madai kuwa Ligi Kuu nchini humo bado inaendelea na wachezaji wamebanwa. Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye amesema jijini Dar es Salaam kwamba Zimbabwe itawasili nchini Tanzania Jumamosi na itashiriki mechi za kundi A kama ilivyokuwa Namibia. "Namibia wametuambia kwamba ligi yao bado inaendelea na wamebanwa sana kwahiyo hawatashiriki, ndio maana tukaichukua Zimbabwe ambayo ni timu imara na ilishaomba tangu awali kushiriki haya mashindano," alisema Musonye. "Zimbabwe ni timu imara na itatoa ushindani,"alisisitiza Musonye na kuongeza kuwa maandalizi ya michuano hiyo imekamilika na mechi ya uzinduzi wa mashindano itakuwa jumamosi baina Tanzania na Rwanda. Zimbabwe itaanza mashindano hayo kwa kucheza na Djibouti Jumapili alasiri kabla ya kuikabili Rwanda Novemba 29. Michuano ya Cecafa inaanza Novemba 25 na kumalizika Desemba 10 kwa kushirikisha timu 12.
No comments:
Post a Comment