Thursday, November 3, 2011

KESHI KOCHA MPYA WA NIGERIA.

SHIRIKISHO la Soka nchini Nigeria-NFF- limemteua beki wa zamani Stephen Keshi kuwa kocha mpya wa timu wa Taifa ya nchi hiyo ikiwa ni siku chache baada ya kumtimua kocha wake Samson Siasia kufuatia kushindwa kwa timu hiyo kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika.Shirikisho hilo limempa kibarua Keshi ambaye alikuwa nahodha wa kikosi hicho katika Kombe la Dunia mwaka 1994 ili kujaribu kukijenga upya kikosi hicho ambacho kinakabiliwa na migogoro mbalimbali pamoja na matokeo mabovu katika kipindi cha miaka miwili.Pamoja na kuomba msamaha kwa umma, mashabiki wa soka wenye hasira wa nchi hiyo walilitaka shirikisho hiyo kumtimua kazi Siasia kwa kusababisha nchi kukosa nafasi michuano hiyo ya Afrika inayotarajiwa kutimua vumbi mapema mwakani.Keshi alitimuliwa kibarua cha kuinoa timu ya Taifa ya Togo mwaka 2006 baada ya kushindwa kuivusha timu hiyo kucheza michuano ya Kombe la Afrika katika kipindi hicho pia alikuwa anaifundisha Mali mwaka huu ambayo nayo imeshindwa kukata tiketi ya kucheza michuano hiyo. Keshi alikuwa sehemu ya kikosi cha Nigeria kilichotwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1994, pia alikuwa anacheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji.

No comments:

Post a Comment