Monday, November 7, 2011

SIMBA KUMUUZA SUNZU KWA DOLA 450,000.

KLABU ya Simba imesema hakuna mchezaji yoyote anayechezea klabu hiyo mwenye thamani ya chini ya dola laki moja. Kauli hiyo imekuja kufuatia baadhi ya magazeti kuandika kuwa kuna klabu inamnyemelea mshambuliaji wake Felix Sunzu katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili. Akizungumza Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema wamezisikia habari hizo za Sunzu kunyemelewa na baadhi ya vilabu hapa. Kamwaga amesema thamani ya mchezaji huyo imepanda kufikia dola 450,000 hivyo kama kuna klabu yoyote inayomuhitaji wao hawatakuwa na matatizo kama wakitoa kiwango hicho cha fedha. Wakati huohuo uongozi wa klabu ya Simba umekemea vikali vitendo vya mashabiki wa timu hiyo waliohudhuria mchezo baina ya timu hiyo na Moro United kwa vitendo vya utovu wa nidhamu walivyovionyesha kwa viongozi wa klabu hiyo. Kamwaga amesema katika mchezo huo baadhi ya mashabiki wasio wastaarabu walikuwa wanatukana viongozi hao matusi kitendo ambacho hakikubaliki katika mchezo wa soka. Amesema klabu hiyo wameomba vyombo vya dola kusaidia kuwachukulia hatua mashabiki kama hao ambao sio tu wanavunja sheria bali pia wanahatarisha amani katika maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment