Thursday, November 24, 2011

TENGA ATETEA KITI CHAKE CECAFA.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA). Tenga amechaguliwa leo (Novemba 24 mwaka huu) bila kupingwa baada ya mpinzani wake Fadoul Hussein wa Djibouti kutotokea kwenye uchaguzi. Kutokana na hali hiyo, mjumbe kutoka Uganda alitoa hoja ya Tenga kupitishwa bila kupingwa, hoja ambayo iliungwa mkono na Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan, Zanzibar, Ethiopia, Burundi na Eritrea. Jumla ya nchi wanachama zilizopiga kura katika uchaguzi uliofanyika hoteli ya New Africa ni kumi na moja, na kila moja ilikuwa na kura moja tu. Kwa upande wa nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya Utendaji kulikuwa na wagombea wanane. Waliopita katika raundi ya kwanza na kura zao kwenye mabano ni Abdiqani Saeed Arab wa Somalia (8),Tariq Atta Salih wa Sudan (8) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Wengine katika raundi ya kwanza na kura walizopata kwenye mabano ni Sahilu Wolde wa Ethiopia (4), Justus Mugisha wa Uganda (4), Tesfaye Gebreyesus wa Eritrea (4), Hafidh Ali Tahir wa Zanzibar (2) na
Abubakar Nkejimana wa Burundi (3). Mjumbe aliyefanikiwa kushinda katika raundi ya pili na kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ni Wolde wa Ethiopia aliyepata kura tano dhidi ya nne za Mugisha na mbili za Gebreyesus. Mwenyekiti anakaa madarakani kwa miaka minne wakati wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanachaguliwa kila baada ya miaka miwili.

No comments:

Post a Comment