Carlos Tevez ameshindwa kufika mazoezini katika klabu yake ya Manchester City siku ya Jumatano asubuhi. Manchester City walitazamia mshambuliaji huyo angekuwepo mazoezini kwenye uwanja wa mazoezi wa Carrington, licha ya kuonekana kwenye picha akiwasili Argentina siku ya Jumanne. Alisafiri kuelekea Amerika Kusini katika siku ambayo iliarifiwa asingepinga mashtaka yaliyomkabili kuhusiana na mechi dhidi ya Bayern Munich. Tevez huenda sasa akakabiliwa na hatua kali zaidi za nidhamu kutokana na kukwepa mazoezi. Wachezaji wengi wa Manchester City kwa sasa wapo nje kwa ajili ya timu zao za taifa lakini Tevez, ambaye hajacheza soka tangu Manchester City ilipoilaza Birmingham mabao 2-0 mwezi wa Septemba, alitakiwa kubakia Manchester kuendelea na mazoezi ya peke yake. Mshambuliaji huyo hayumo katika kikosi cha Argentina kitakachopambana dhidi ya Bolivia na Colombia, wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment