Friday, February 3, 2012

FIFA YAOMBA RIPOTI YA MAUAJI MISRI.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetaka taarifa kamili juu ya vurugu zilizotokea nchini Misri na kupelekea vifo vya watu wapatao 74. FIFA imeomba mamlaka husika kufafanua kwa kina chanzo haswa cha kuzuka kwa vurugu hizo wakati wa mchezo baina ya Al Ahly na Al Masry Jumatano. Katika barua aliyomwandikia rais wa Chama cha Soka cha Misri-EFA Samir Zaher rais wa FIFA Sepp Blatter amesema kuwa ni tukio la kuhuzunisha sana na lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kuhakikisha vitendo kama hivyo havitokei tena. Blatter aliendelea kusema katika barua hiyo kuwa mchezo wa mpira wa miguu ni burudani hivyo hatupaswi kuruhusu watu wachache wavuruge amani ya mchezo huo. Wakati huohuo salamu za rambirambi zimeendelea kumiminika ambapo Zhang Jilong anayekaimu nafasi ya rais wa Shirikisho la Soka barani Asia-AFC ametuma salamu zake za rambirambi kwa EFA. Katika salamu zake hizo Jilong amesema kuwa wako pamoja na familia na marafiki walifariki katika janga hilo kubwa kutokea katika ulimwengu wa soka na kuomba wahusika wachuliwe hatua mara moja ili kulinda heshima ya mchezo huo.

No comments:

Post a Comment