Wednesday, February 15, 2012

FIFA YASUBIRI MAELEZO YA TTFF.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA imethibitisha kuwa inasubiri maelezo kuhusu fedha za msaada kufuatia tetemeko la ardhi nchini Haiti ambazo zimeshindwa kufika huko baada ya kutumwa kupitia Shirikisho la Soka nchini Trinidad na Tobago-TTFF. FIFA imesema fedha hizo zilitumwa TTFF mwaka 2010 ambapo ziliombwa na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FIFA Jack Warner ambaye katika kipindi hicho alikuwa kiongozi wa Vyama vya Soka vya Amerika ya Kaskazini, Kati na Caribbean-Concacaf. Katika taarifa yake FIFA imesema ilituma kiasi cha dola 250,000 kwenda TTFF lakini Shirikisho la Soka nchini Haiti limedai limepata dola 60,000 pekee. FIFA imesema bado haijapata maelezo yoyote kuhusu kilichotokea kwa kiasi dola 190,000 zilichobakia na tayari wamezuia misaada yote inayokwenda TTFF mpaka hapo watakapopata maelezo ya kina juu ya sula hilo. Haiti ilikumbwa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa magnitude 7.0 ambalo liliua zaidi ya watu 300,000 na kuacha wengine zaidi ya milioni 1.5 wakiwa hawana makazi miaka miwili iliyopita.

No comments:

Post a Comment