Tuesday, March 27, 2012

MADRID, CHELSEA ZATENGENEZA MAZINGIRA MAZURI YA KUSONGA MBELE.

KLABU za Chelsea na Real Madrid jana usiku zimefanikiwa kushinda michezo yao ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutinga Nusu Fainali. Salomon Kalou aliunganisha krosi ya Fernando Torres dakika ya 75, kuipatia Chelsea ushindi wa 1-0 dhidi ya Benfica jijini Lisbon, Ureno, huo ukiwa ushindi wa kwanza ugenini kwa timu hiyo kwenye mashindano hayo msimu huu. Nchini Cyprus, Karim Benzema alifunga bao la kichwa dakika ya 74 akimalizia krosi safi iliyopigwa na Kaka, huku Kaka nae akifunga bao la pili wakati Benzema alipoongeza lingine dakika ya 82 na kuihakikishia ushindi Real Madrid wa mabao 3-0 dhidi ya APOEL Nicosia. Michezo ya marudiano baina ya timu hizo itapigwa Aprili 4 mwaka huu ambapo Chelsea wataikaribisha Benfica katika Uwanja wa Stamford Bridge huku Madrid wakiwakaribisha APOEL katika Uwanja wa Santiago Bernabeu nchini Hispania. Michezo mingine ya kwanza ya robo fainali inatarajiwa kuendelea tena leo ambapo mabingwa watetezi wa michuano hiyo Barcelona watachuana na AC Milan huku Olympic Marseille wakiikaribisha Bayern Munich huko Ufaransa.

No comments:

Post a Comment