Tuesday, March 27, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

VITA VPL YAHAMIA MORO UNITED, VILLA
Timu za Moro United na Villa Squad ambazo ziko kwenye vita ya kukwepa kushuka daraja katika Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinapambana kesho (Machi 28 mwaka huu) kwenye moja kati ya mechi mbili za siku hiyo. Mechi hiyo namba 153 itachezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili. Moro United iko nafasi ya 11 ikiwa na pointi 18 wakati Villa Squad iko nafasi ya 14 kwa pointi zake 14. Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa mzunguko na sh. 5,000 kwa jukwaa kuu. Mwamuzi atakuwa Andrew Shamba akisaidiwa na Samson Kobe na Idd Mikongoti wote wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Arthur Mambeta wa Dar es Salaam wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Emmanuel Chaula kutoka mkoani Rukwa. Mechi nyingine ya Machi 28 mwaka huu itakayochezeshwa na mwamuzi Judith Gamba wa Arusha itakuwa kati ya Ruvu Shooting itakayoikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani. Gamba katika mechi hiyo namba 150 atasaidiwa na Saada Tibabimale kutoka Mwanza na Hellen Mduma wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa akiba ni Juma Safisha wa Pwani wakati Kamishna ni Hamis Kissiwa wa Dar es Salaam. Mechi za Machi 31 mwaka huu ni Coastal Union dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi ya African Lyon na Simba.

RHINO, POLISI DAR KUANZA FAINALI FDL
Timu za Rhino Rangers ya Tabora na Polisi Dar es Salaam zitapambana Machi 31 mwaka huu katika moja ya mechi za ufunguzi wa fainali za Ligi Daraja la Kwanza zitakazochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Kila siku zitachezwa mechi mbili, moja ikianza saa 8 mchana wakati ya pili ni saa 10 jioni ambapo fainali hiyo itamalizika Aprili 22 mwaka huu kwa timu tatu za kwanza kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao- 2012/2013. Morogoro imepewa uenyeji baada ya kulipa sh. milioni 20.5 kati ya sh. milioni 25 zilizotakiwa. Sh. milioni 4.5 zilizobakia imekubaliana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwa itazilipa moja kwa moja kwenye huduma zitakazotumiwa na wasimamizi wa fainali hizo. Mkoa mwingine ulioomba uenyeji ulikuwa Mbeya. Lakini wenyewe hadi Machi 26 mwaka huu ambayo ilikuwa siku ya mwisho kufanya malipo ulikuwa umeingiza kwenye akaunti ya TFF sh. milioni 15. Upangaji ratiba (draw) ulifanyika jana (Machi 26 mwaka huu) kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kushuhudiwa na viongozi wa timu saba kati ya tisa zinazocheza fainali hizo. Mechi ya pili siku ya ufunguzi itakuwa kati ya Trans Camp na Mbeya City Council. Aprili Mosi ni Tanzania Prisons na Polisi Morogoro zitakazocheza mchana wakati jioni ni Mgambo Shooting na Mlale JKT. Aprili 2 mwaka huu ni Polisi Tabora vs Rhino Rangers (mchana) na Polisi Dar es Salaam vs Trans Camp (jioni). Aprili 3 mwaka huu ni Mbeya City Council vs Tanzania Prisons (mchana) na Polisi Morogoro vs Mgambo Shooting (jioni). Aprili 5 mwaka huu ni Polisi Tabora vs Mlale JKT (mchana) wakati jioni ni Rhino Rangers vs Trans Camp. Aprili 6 mwaka huu Polisi Dar es Salaam vs Mbeya City Council (mchana) wakati jioni ni Tanzania Prisons vs Mgambo Shooting. April 8 mwaka huu ni Mlale JKT vs Polisi Morogoro (mchana) wakati jioni itakuwa Polisi Tabora vs Polisi Dar es Salaam. Aprili 9 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Rhino Rangers (mchana) wakati jioni ni Trans Camp vs Tanzania Prisons. Aprili 11 mwaka huu ni Mbeya City Council vs Polisi Tabora (mchana) na Mlale JKT vs Rhino Rangers (jioni). Aprili 12 mwaka huu Polisi Dar es Salaam vs Mgambo Shooting (mchana) na Polisi Morogoro vs Trans Camp (jioni).

LIGI YA TAIFA KUANZA APRILI 22
Kamati ya Mashindano ya TFF iliyokutana Machi 24 mwaka huu imepitisha michuano ya Ligi ya Taifa Ngazi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa ianze Aprili 22 mwaka huu kwenye vituo vitatu tofauti. Wakati Machi 26 mwaka huu ndiyo ilikuwa mwisho kwa vyama vya mikoa kuwasilisha TFF majina ya mabingwa wao, ni mikoa minne tu iliyomudu kufanya hivyo kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya TFF. Mikoa hiyo na mabingwa wake kwenye mabano ni Kigoma (Kanembwa FC ya Kibondo), Ruvuma (Mighty Elephant ya Songea), Kilimanjaro (Forest FC ya Siha) na Dodoma (CDA ya Dodoma Mjini).Hivyo Kamati ya Mashindano imeongeza muda hadi Aprili 9 mwaka huu kwa mikoa  ambayo haijawasilisha majina ya mabingwa wao iwe imefanya hivyo. Kwa itakayoshindwa ndani ya muda hiyo, mabingwa wao hawatapata fursa ya kucheza ligi hiyo. Kamati imetoa pongezi kwa mikoa hiyo minne kwa kuhakikisha imechezesha ligi yao kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya TFF. Pia imepanga makundi matatu ya ligi hiyo. Kundi A lina mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Lindi na Mtwara. Kundi B lina mabingwa wa mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Singida na Dodoma. Kundi C ni Dar 1, Dar 2, Dar 3, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. TFF inakaribisha maombi ya uenyeji kwa kila kundi. Taarifa rasmi itatumwa kwa vyama mikoa kueleza masharti ya kutimiza kabla ya mkoa kupewa kituo cha ligi hiyo. Mshindi katika kila kundi na washindwa bora (best losers) wawili kutoka kwenye makundi yenye timu nane watapanda daraja msimu ujao kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Pia timu zinatakiwa ziwe zimefanya usajili wa wachezaji kufikia Aprili 10 mwaka huu wakati Aprili 11-18 itakuwa ni kipindi cha kutangaza majina na pingamizi.

KOMBE LA FA KUANZA TENA MSIMU UJAO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limerejesha tena mashindano ya Kombe la FA (TFF) kuanzia msimu ujao 2012/2013 ambapo bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho. Timu zinazotakiwa kushiriki michuano hiyo itakayochezwa kwa mtindo wa mtoano ni zilizosajiliwa ambapo katika maombi yao ni lazima ziambatanishe nakala ya hati ya usajili wa klabu ambayo itatakiwa kuidhinishwa na chama cha mpira wa miguu cha wilaya. Ada ya fomu ya maombi ya kushiriki ni sh. 20,000 wakati ada ya mashindano ni sh. 200,000. Usajili wa wachezaji katika Kombe la FA ni ule ule mmoja wa kalenda ya usajili ya TFF ambapo unaanza Juni Mosi na kumalizika Septemba 10.

No comments:

Post a Comment