Monday, April 2, 2012

NYOTA WA ZAMANI WA LAZIO AFARIKI DUNIA.

MCHEZAJI nyota wa zamani kimataifa wa Italia ambaye amewahi pia kuzichezea klabu za Lazio na New York Cosmos, Giorgio Chinaglia amefariki dunia kutokana na matatizo ya ugonjwa wa moyo. Katika taarifa iliyotolewa na mtoto wa kiume wa mchezaji huyo aitwae Antony amesema kuwa Chinaglia alifariki akiwa nyumbani kwake Naples, Florida, Marekani ambapo alikuwa akifanya kazi katika kituo kimoja cha radio nchini humo. Klabu ya Lazio pia ilitangaza kifo cha Chinaglia ambaye alikuwa akiishi Marekani toka alipotuhumiwa kushirikiana na kikundi cha wahalifu ambao walikuwa wakitaka kuinunua Lazio mwaka 2006. Chinaglia aliisaidia Lazio kushinda taji lake la kwanza la Ligi Kuu nchini Italia mwaka 1974 ambapo baadae aliteuliwa kuwa rais wa klabu hiyo. Mwaka 1976 alijiunga na klabu ya Cosmos ya Marekani akicheza pamoja na gwiji wa soka wa Brazil Pele pamoja na nyota wa Ujerumani enzi hizo Franz Beckenbauer na pia aliwamo katika kikosi cha Italia kilichoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1974.

No comments:

Post a Comment