Friday, May 11, 2012

BARCELONA YAMKINGIA KIFUA MESSI.

KLABU ya Barcelona imemtetea mshambuliaji wake nyota Lionel Messi kuhusiana na tuhuma za ubaguzi dhidi ya mchezaji mwenye asili ya kiafrika wa klabu Real Madrid miaka michache iliyopita. Kiungo huyo wa kimataifa wa Uholanzi, Royston Drenthe ambaye kwasasa anacheza kwa mkopo katika klabu ya Everton alikaririwa na gazeti moja la nchini kwao akidai kuwa mshambuliaji huyo alikuwa akimwambia maneno ya kibaguzi katika baadhi ya michezo ambayo timu hizo zilikutana katika Ligi Kuu ya Hispania. Katika taarifa yake Barcelona ilisema kuwa hawadhani kama tuhuma hizo zina ukweli wowote kwani mchezaji huyo amekuwa na nidhamu ya hali ya juu na amekuwa akiheshimu wachezaji wa timu pinzani ambao amekuwa akicheza nao. Drenthe katika maelezo yake alidai kuwa Messi amekuwa akitumia neno ‘negro’ ambalo hutumika kumdhalilisha mtu mweusi katika kipindi ambacho bado alikuwa akicheza soka nchini Hispania. Tabia za kuwabagua wachezaji weusi hivi sasa inapigwa vita barani Ulaya ambapo hivi karibuni mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez alifungiwa michezo nane baada ya kukutwa na hatia ya ubaguzi kwa mchezaji wa Manchester United Patrice Evra mwanzoni mwa msimu huu.

No comments:

Post a Comment