MAJESHI ya kiislamu ambayo yanashikilia miji iliyopo Kaskazini mwa Mali, wametangaza kuwa wanaanza kutumia sheria za kiislamu-Sharia katika miji hiyo wanayoshikilia na kuwaambia wakazi wa maeneo hayo kuzifuata sheria hizo ambazo pia zinakataza mchezo wa mpira wa miguu. Wakazi wanaokaa maeneo ya mji wa Tombouctou siku ya kesho watauaga mchezo wao wanaoupenda ambapo mmoja wa viongozi wa kijeshi wanaoshikilia upande huo amesema kuwa sasa mchezo wa soka utachezwa nje ya mipaka eneo hilo na atakayekiuka amri hiyo atachukuliwa hatua kali. Mbaya zaidi sheria hizo za kiislamu zinakataza pia mashabiki wa soka kuangalia mchezo huo katika luninga zao. Mbali na kukataza mchezo wa soka, sheria hizo pia zinakataza mtu yoyote kuzungumza na mtu ambaye ana jinsia tofauti na yake ambapo wanawake wameamriwa kuvaa nguo ambazo zinafunika sehemu kubwa ya miili yao wakati wanaume wametakiwa kufuga ndevu. Mali imetumbukia katika mgogoro usiokuwa wa kawaida wa kisiasa na kijeshi baada ya chama kiitwacho National Movement for the Liberation of Azawad (MNLA) kuigawa nchi hiyo katika pande mbili za Kaskazini na Kusini April Mwaka huu.
No comments:
Post a Comment