Tuesday, May 8, 2012

WAZEE YANGA WAMCHARUKIA NCHUNGA.

MGOGORO katika klabu ya soka ya Yanga unaonekana kushika kasi baada ya wazee wa klabu hiyo kuibuka tena na kumuonya Mwenyekiti wake Nchunga kutomfukuza mchezaji yoyote kwa madai ya kuihujumu timu. Kauli ya wazee hao imekuja kufuatia Nchunga kutangaza kuwafukuza baadhi ya wachezaji kwa madai ya kuhujumu mchezo baina ya timu hiyo na Simba ambapo ilifungwa mabao 5-0 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mara baada ya mchezo huo Nchunga alikaririwa na vyombo vya habari akidai kuwa kufungwa kwa timu hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji ambao alidai walikuwa wanaihujumu timu ambapo atachukua hatua kali ikiwemo kuwafukuza wachezaji watakaogundulika kufanya hujuma hiyo. Wazee hao ambao waliwakilishwa na katibu wao Ibrahim Akilimali walifunguka kwa kusema kuwa Nchunga asikwepe majukumu kwa kuwatupia lawama wachezaji kwani waliingia uwanjani wakiwa hawako katika hali ya kimchezo kutokana na kutopewa posho zao za wiki mbili huku wengine wakidai pesa zao za usajili mpaka leo. Mapema kabla ya mchezo huo mzee Akilimali alidai kuwa wachezaji waligoma kwenda uwanjani kushinikiza kupewa posho zao hizo mpaka wanachama wafanyabiashara wa klabu hiyo Ahmed Seif na Abdallah Bin Kleb walipookoa jahazi kwa kuwapa wachezaji posho za laki tatu ndio wakakubali kuingia uwanjani. Wafanyabiashara hao walitoa fedha hizo kuhofia timu kama isingeweza kuingia uwanjani kwenye mchezo huo kungekuwa na uwezekano mkubwa wa kufungiwa au kushushwa daraja na Shirikisho la Soka nchini-TFF. Mzee Akilimali aliendelea kusema kuwa ili kulinda heshima yake Nchunga anapaswa kujiuzulu wadhfa huo na kupisha wengine ambao wana uwezo zaidi wa kuongoza soka ili kuiwezesha Yanga kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara. “Akumbuke alikojikwaa asikumbuke alikoangukia ni wazi amewachukiza wazee angetafuta namna ya kutafuta suluhu kwani wazee hao ni dawa na muhimili mkubwa katika jamii” alisema Akilimali.

No comments:

Post a Comment