Wednesday, June 6, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KIINGILIO MECHI YA TAIFA STARS, GAMBIA 3,000/-
Kiingilio cha chini ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Gambia (The Scorpions) itakayochezwa Jumapili (Juni 10 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 3,000. Watazamaji watakaolipa kiingilio hicho ni watakaokaa kwenye viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo ni 36,693 kati ya jumla ya viti 57,558 vilivyopo katika uwanja huo wa kisasa. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ni sh. 5,000. Kwa upande wa VIP C watalipa sh. 10,000 wakati VIP B ni sh. 20,000. Kiingilio kwa jukwaa la VIP A ambalo linachukua watazamaji 748 tu ni sh. 30,000 kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni. Tiketi zitaanza kuuzwa Jumamosi (Juni 9 mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi kwenye vituo vya Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio na Samora, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Soko Kuu la Kariakoo na Uwanja wa Taifa. Siku ya mechi pia mauzo yatafanyika katika vituo hivyo na baadaye kuhamia Uwanja wa Taifa.

GAMBIA YATARAJIA KUINGIA LEO DAR ES SALAAM
Timu ya Taifa ya Gambia (The Scorpions) inatarajia kuwasili nchini wakati wowote kuanzia leo (Juni 6 mwaka huu) tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars. Kamati ya Maridhiano inayoendesha Chama cha Soka Gambia (GFA) hadi leo mchana ilikuwa haijatuma taarifa rasmi kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) juu ya ujio wake. Lakini vyombo vya habari vya Gambia vimeripoti kuwa timu hiyo ikiwa na wachezaji 23 na viongozi tisa ilitarajiwa kuondoka huko leo kuja Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na washabiki wengi nchini. Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa GFA aliyekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo, Bakary Balder, msafara wa timu hiyo utaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo, Malang Jassey. Mbali ya Jassey, viongozi wengine katika msafara huo ni Ofisa Utawala wa timu Modou Sowe, Kocha Luciano Machini, makocha wasaidizi Peter Bonu Johnson na Lamin Sambou, Kocha wa makipa Alhagie Marong, mtaalamu wa tiba mbadala (physiotherapist) Pa Matarr Ndow, Mtunza vifaa Sanna Bojang na Daktari wa timu Kalifa Manneh. Wachezaji ni Musa Camara, Abdou Jammeh, Momodou Futty Danso, Lamin Basmen Samateh, Ousman Koli, Pa Saikou Kujabi, Mustapha Kebba Jarju, Yankuba Mal Ceesay, Demba Savage, Saihou Gassama, Alieu Darboe, Momodou Ceesay, Pa Modou Jagne, Tijan Jaiteh, Bubacarr Sanyang, Christopher Allen, Musa Yaffa, Sulayman Marr, Mamut Saine, Hamsa Barry, Ali Sowe, Omar Colley na Saloum Faal.

PROGRAMU YA TAIFA STARS KWA MECHI YA GAMBIA

JUMATANO JUNI 6
01.00 asubuhi Mazoezi- Uwanja wa Karume
10.00 jioni Mazoezi- Uwanja wa Taifa

ALHAMISI JUNI 7
10.00 jioni Mazoezi- Uwanja wa Taifa

IJUMAA JUNI 8
10.00 jioni Mazoezi- Uwanja wa Taifa

JUMAMOSI JUNI 9
04.00 asubuhi Mkutano na Waandishi wa Habari- Ukumbi wa TFF
11.00 jioni Mazoezi- Uwanja wa Taifa

No comments:

Post a Comment