DESCHAMPS KOCHA MPYA UFARANSA.
 |
Didier Deschamps. |
SHIRIKISHO la Soka la Ufaransa-FFF limemteua nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo Didier Deschamps kuwa meneja mpya wa kikosi cha nchi hiyo. Deschamp mwenye umri wa miaka 43 alioachia nafasi yake kama kocha wa klabu ya Olympique Marseille na nafasi yake kuchukuliwa na kocha Laurent Blanc ambaye alijiuzulu wadhifa wake wa kuifundisha Ufaransa baada ya timu kutolewa katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Ulaya. Mchezo wa kwanza wa Deschamps akiwa kocha wa timu hiyo utakuwa dhidi ya mabingwa wa soka wa Amerika Kusini, Uruguay mchezo ambao utachezwa jijini La Havre Agosti 15 mwaka huu. Kocha huyo anaweza kuwakosa nyota wake kadhaa kama Samir Nasri, Jeremy Menez, Hatem Ben Arfa na Yann M’Villa baada ya FFF kuwachukuliwa hatua ya kinidhamu kutoka tabia walizozionyesha wakati wa michuano ya Ulaya. Nasri alimtolea maneno makali mwandishi wakati Menez naye alifanya kama hivyo kwa nahodha wa kikosi chao Hugo Lloris huku Ben Arfa yeye aligombana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Blanc wakati M’Villa yeye anashutumiwa kwa kutompa mkono kocha wake wakati alipotolewa ili ampishe mwenzake katika mchezo wao wa mwisho. Ufaransa itaanza kampeni zake za kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 wakiwa na mchezo wa ugenini dhidi ya Finland Septemba 9 mwaka huu kabla ya kuwakaribisha Belarus siku nne baadae. Katika kundi I ambalo Ufaransa wamepangwa pia wako na mabingwa watetezi Hispania na Georgia.
No comments:
Post a Comment