Friday, July 27, 2012

FIFA YAMSIMAMISHA TENA BIN HAMMAM.

Mohamed Bin Hammam.
ALIYEKUWA mgombea urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Mohamed Bin Hammam amesimamishwa tena na shirikisho hilo ikiwa ni wiki moja tu baada ya kifungo chake cha maisha kutenguliwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo-CAS. Katika taarifa iliyotolewa na FIFA imesema kuwa Bin Hammam amefungiwa kwa siku 90 wakati Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo ikipitia na kukusanya ushahidi zaidi juu ya tuhuma za kujaribu kwanunua viongozi wan chi za Caribbean katika uchaguzi uliopita. Kamati hiyo pia itachunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha wakati Bin Hammam akiwa kiongozi wa Shirikisho la Soka barani Asia-AFC. Bin Hammam ambaye ni raia wa Qatar tayari amesimamishwa kwa muda wa siku 30 na AFC ili kupisha uchunguzi kufanyika ambapo wiki iliyopita CAS ilitengua adhabu ya kufungiwa maisha na kusema kuwa FIFA haikuwa na ushahidi wa kutosha juu ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili. Bin Hammam ambaye alikuwa mjumbe wa zamani wa kamati ya utendaji wa FIFA alichuana na Sepp Blatter katika kinyang’anyiro cha urais mwaka uliopita lakini alijitoa baada ya kutuhumiwa kuwahonga dola 40,000 kila mjumbe wa nchi za Caribbean ili wampigie kura katika uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment