Thursday, July 12, 2012

HAVELANGE ATAJWA KATIKA KESI YA RUSHWA YA MABILIONI.

Joao Havelange.
WAENDESHA mashitaka nchini Switzerland wameonyesha hati inayowataja rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Joao Havelange na Ricardo Teixeira ambaye amewahi kuwa mkwewe kuhusika na hongo ya mamilioni ya dola kwa ajili ya mikataba ya Kombe la Dunia. Viongozi hao wa soka wanaotoka nchini Brazil wametajwa kwa mara ya kwanza katika kesi ambayo ilikuwepo katika miaka ya tisini lakini itaongeza shinikizo kwa FIFA kuonyesha kama kweli wanataka kujisafisha. Katika hati hiyo iliyotolewa na kutoka ofisi ya waendesha mashitaka katika mkoa wa Zug nchini humo, ilionyesha kuwa Teixeira pamoja na Havelange walikana kuhusika na tuhuma hizo na rais huyo wa zamani hakuwa na maoni juu ya shutuma za maadili ya makosa ya jinai. Waendesha mashitaka hao wanadai kuwa Havelange ambaye amekuwa kiongozi wa FIFA kuanzia mwaka 1974 mpaka 1998 alipokea malipo ya kiasi cha dola milioni 1.53 Machi mwaka 1997 kutoka kampuni moja inayojihusisha na masuala ya michezo ya ISL. ISL walikuwa wakiuza haki za biashara ya matangazo ya michuano ya Kombe la Dunia kwa niaba ya FIFA lakini baadae kampuni ilifilisiwa kutokana na deni la dola milioni 300 mwaka 2001. Teixeira ambaye aliliongoza Shirikisho la Soka la Brazil kuanzia mwaka 1989 mpaka alipoachia madaraka hayo mapema mwaka huu yeye alichukua kiasi cha dola milioni 12.7 kati ya mwaka 1992 na 1997 kwa mujibu ya waendesha mashtaka hao. Watuhumiwa wote wawili hawakupatikana mara moja kuzungumzia tuhuma hizo zinazowakabili mara moja.

No comments:

Post a Comment