METSU AKABIDHIWA MIKOBA ILIYOMSHINDA MARADONA AL WASL.
 |
| Bruno Metsu. |
KOCHA wa zamani wa timu za taifa za Senegal na Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE, Bruno Metsu ameteuliwa kuifundisha klabu ya Al Wasl yenye maskani yake jijini Dubai akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Diego Maradona. Maradona ambaye ni raia wa Argentina alitimuliwa wiki iliyopita akiwa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja kati ya miwili aliyosaini kufutia kuvurunda kwa timu hiyo msimu uliopita na kukosa kombe lolote. Taarifa ya klabu hiyo ambayo ilitumwa katika mtandao wa kijamii wa twitter imesema kuwa Metsu ambaye ana umri wa miaka 58 raia wa Ufaransa amepewa mkataba wa miaka miwili ambapo maelezo zaidi juu ya suala hilo watalizungumzia katika mkutano na waadishi wa habari ambao utaitishwa siku chache zijazo. Maradona alitimuliwa baada ya Al Wasl kumaliza katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo inayojulikana kama Pro League ambayo hushirikisha timu 12 pekee. Metsu aliifundisha UAE na kufanikiwa kunyakuwa Kombe la Gulf mwaka 2007 na pia alikiongoza kikosi cha Senegal katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2002 ambapo aliiwezesha timu hiyo kuwafunga mabingwa watetezi Ufaransa bao 1-0 katika mchezo wa ufunguzi kabla ya kuifikisha timu katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment