Thursday, July 12, 2012

SAINTFIET APONDA WAANDISHI KUTOMUELEWA UFUNDISHAJI WAKE.

Kocha wa Yanga Tom Saintfiet(katikati) akizungumza na waandishi wa habari kama wanavyoonekana pichani katika  Makao Makuu ya klabu hiyo mtaa wa Twiga na Jangwani. (Picha kwa hisani ya Bin Zubery.)
KOCHA wa klabu ya Yanga, Tom Saintfiet ametetea aina ya ufundishaji aliyotumia wakati wa mchezo wa kirafiki baina ya timu hiyo na JKT Ruvu uliofanyika Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kauli hiyo imekuja kufuatia kikosi cha timu hiyo kuonyesha mchezo wa kujihami karibu muda wote wa mchezo dhidi ya JKT ambao pamoja na hivyo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 mabao ambayo yalifungwa na Nadir Haroub na Said Bahamuzi. Pamoja na ushindi huo wadau pamoja na mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza waliponda aina mchezo ambao timu ilicheza kwani wameshazoea timu hiyo ikiwa inacheza mchezo wa kushambulia zaidi wanapokuwa uwanjani. Baadhi ya mashabiki hao walidiriki kusema kwa nyakati tofauti kwamba kocha huyo anawachanganya wachezaji kwa mfumo wake huo mpya na kuhofia endapo timu itakapokutana na timu ngumu kama Simba na Azam inaweza kuwa vigumu kuibuka na ushindi. Akizungumza na waandishi wa habari, Saintfiet aalitetea mfumo wake huo kwamba wachezaji wake wameuelewa vizuri tofauti na baadhi ya magazeti yalivyodai kwamba mfumo huo wachezaji uliwachanganya. “Nadhani mfumo nilioutumia katika mchezo dhidi ya JKT uliwachanganya waandishi na sio wachezaji wake kama baadhi ya magazeti yanavyosema”. Alisema kocha huyo akifafanua jambo hilo kwa waandishi wa habari. Saintfiet amesema kuwa mfumo aliotumia katika mchezo ulikuwa safi na walikuwa wamekubaliana na benchi lake la ufundi pamoja na wachezaji ambao walionyesha kuufahamu vyema ndio maana wakapa matokeo waliyoyapata. Amesema kuwa mfumo huo sio mgeni sana kwani umetumiwa katika michuano iliyopita ya Ulaya pamoja na Kombe la Dunia lililopita ambapo timu kama Hispania, Ujerumani, Uholanzi na hata Ghana wamekuwa wakiutumia na kufanikiwa katika michezo yao. Kocha huyo aliwaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwani ina wachezaji wazuri wenye kiwango kizuri na upeo mkubwa wa kuelewa aina ya mbinu ambazo atakuwa akiwapa wachezaji hao.

No comments:

Post a Comment