Sunday, July 29, 2012

SHEVCHENKO AAMUA KUKIMBILIA KWENYE SIASA.

Andriy Shevchenko.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea Andriy Shevchenko ametangaza kustaafu kucheza soka rasmi ili aweze kujishughulisha na nmasuala ya siasa. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ukraine mwenye miaka 35 alithibisha taarifa hizo ambazo zilitolewa katika mtandao wa klabu ya Dynamo Kiev ambayo alikuwa akicheza. Shevchenko amecheza mechi 111 kwa nchi yake ambapo mara ya mwisho ilikuwa katika michuano ya Ulaya iliyomalizika mapema mwezi huu ambapo Ukraine ilifungwa bao 1-0 na Uingereza. Mshambuliaji huyo aliibukia katika klabu ya Dynamo mwaka 1994 na baadae kuhamia klabu ya AC Milan mwaka 1999 ambapo alifanikiwa kushinda taji la Ligi ya mabingwa ya Ulaya mwaka 2003 na klabu hiyo huku yeye akiwa ndio nyota wa mchezo baada ya kushinda penati ya mwisho. Akiwa na miaka 29 Shevchenko alihamia katika klabu ya Chelsea ambayo ilikuwa ikifundishwa na Jose Mourinho mwaka 2006 kwa ada paundi milioni 30 lakini hakupata mafanikio katika misimu miwili aliyochezea klabu hiyo na kuamua kurejea AC Milan ambapo nako hakukaa sana kabla ya kuamua kurejea Dynamo mwaka 2009. Shevchenko amefunga mabao 48 na kurekodi ya mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika timu ya taifa ya nchi hiyo huku akikiongoza kikosi cha nchi hiyo kilichofika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006 na pia aliwahi kutunukiwa tuzo ya mchezaji bora barani Ulaya mwaka 2004.

No comments:

Post a Comment