MCHEZO wa soka umeingia katika historia mpya baada ya Bodi ya Kimataifa ya mchezo-IFAB ambao ndio watungaji wa sheria kuruhusu mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli na wanawake kuvaa hijabu kwa wachezaji soka waislamu. Mbali na hizo IFAB pia imepitisha ombi la kutumia waamuzi watano katika mchezo mmoja tofauti na waamuzi watatu kama ilivyokuwa hapo awali ambapo waamuzi wawili waliongezeka watakuwa wakikaa pembeni ya magoli. Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA kwa pamoja na IFAB walitangaza taarifa hizo baada ya kikao cha kujadili masuala hayo kilichofanyika jijini Zurich, Switzerland. FIFA imesema kuwa itaanza kutumia mfumo huo katika michuano ambayo inashirikisha timu saba ya Klabu Bingwa ya Dunia itakayofanyika nchini Japan Desemba mwaka huu huku wakiwa na mipango pia ya kuitumia katika michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka 2013 pamoja na Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil. Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa wanataka mfumo huo ufanye kazi kwa asilimia 150 na sio 90 mpaka itakapofika michuno ya Kombe la Dunia ambapo shirikisho litatumia mifumo yote miwili ambayo inaitwa Hawk-Eye na GoalRef katika michuano ya Japan. Ligi Kuu nchini Uingereza inatarajiwa kutumia mfumo mojawapo kati ya hiyo katika msimu ujao wa ligi hiyo ambapo gharama zake zinafikia kiasi cha dola 250,000 kwa kufunga mfumo huo kwenye uwanja mmoja. IFAB pia imepitisha uvaaji wa Hijabu kwa wanawake kwenye mchezo huo baada ya timu ya kamati ya afya ya FIFA kuridhia kwamba vazi hilo halina madhara yoyote kiafya kwa mtumiaji wakati wa mechi. Hiyo ni habari njema kwa makamu wa rais wa FIFA Prince Ali wa Jordan ambaye ndio alikuwa akiendesha kampeni vazi hilo likubaliwe baada ya shirikisho hilo kulipiga marufuku mwaka 2007 ambapo nchi kama Iran na Saudi Arabia wachezaji wake walikuwa wakivaa.
MIFUMO HIYO INAFANYA KAZI VIPI?
Mfumo wa ‘Hawk-Eye’ au ‘Jicho la Mwewe’ wenyewe unategemea kamera sita zikiangaza kila lango na kuufuata mpira uwanjani, kasha kiufundi huwa teknologia hiyo inatambua mahali halisi mpira ulipo kuipitia utaalamu unaojulikana kwa lugha ya kigeni kama ‘Triangulation’. Ikiwa mpira utavuka mstari wa goli, basi ujumbe kupitia mawimbi ya redio hutumwa moja kwa moja hadi katika saa ya mkononi aliyovaa mwamuzi kumwarufu kwamba bao limefungwa na kama kanuni za FIFA zinavyohitaji utaratibu mzima hauchukui zaidi sekunde moja. Mfumo wa ‘GoalRef’ nao unatumia kifaa kinachojulikana kwa lugha ya kigeni kama ‘microchip’ ambacho hubandikwa katika mpira unaotumiwa na kwa kutumia mawimbi ya sumaku karibu na goli. Iwapo mabadiliko fulani yatajitokeza katika mawimbi kupitia mpira kuvuka mstari, teknolojia inaamua kama hilo ni goli na kasha kwa njia ya elektroniki mwamuzi hujulishwa katika muda usiozidi sekunde moja kwamba goli limefungwa.
No comments:
Post a Comment