Friday, August 3, 2012

NGASSA ATAMBULISHWA RASMI SIMBA.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange marufu kama Kaburu akimtambulisha Mrisho Ngassa mbele ya waandishi wa habari katika Makao Makuu ya klabu hiyo Msimbazi.
ALIYEKUWA mshambuliaji wa Azam Mrisho Ngassa ametambulishwa rasmi mbele ya waandishi wa habari katika klabu yake mpya ya Simba ambayo imeingia naye mkataba wa mwaka mmoja. Ngassa ambaye katika siku za karibuni amekuwa gumzo miongoni mwa wapenzi wa soka kutokana na vitendo alivyovionyesha katika michuano ya Kombe la Kagame na kupelekea Azam kuamua kumuuza. Awali ilitarajiwa mchezaji huyo angeuzwa kwenda klabu ambayo inasemekana ana mapenzi nao ya Yanga lakini katika hali ya kushangaza Azam iliamua kumpeleka Simba kitendo mwenyewe alidai hakuridhishwa nacho. 
Ngassa akionyesha jezi aliyokabidhiwa Simba.
Akizungumza na waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange-Kaburu amesema kuwa uhamisho wa mchezo huyo umetokana na maelewano ya pande zote tatu yaani Azam, Simba na Ngassa mwenyewe yaliyofikiwa. Kaburu amesema kuwa mchezaji huyo amekabidhiwa jezi namba 16 na anatarajiwa kuonekana katika michezo mbalimbali ya timu hiyo ikiwemo ya kirafiki na Ligi Kuu ambayo inatarajiwa kuanza baadae mwezi huu. Kaburu aliwaomba washabiki wa Simba kumpokea mchezaji huyo kwa mikono miwili kwani amekwenda hapo ili kufanya kazi na kuiletea klabu hiyo vikombe zaidi hivyo wawe na imani nae. Ngassa mwenyewe akihojiwa amesema kuwa ameenda katika klabu hiyo kufanya kazi na kuahidi kuifanyia makubwa klabu hiyo na kuwaomba viongozi na mashabiki wa klabu hiyo kumpa ushirikiano ili aweze kufikia nia yake. Wakati huohuo badhi ya mashabiki wachache waliohojiwa kuhusiana na suala hilo wameonyesha kutokuwa na imani na Ngassa kama ataitumikia klabu hiyo kwa moyo kutokana na kuonyesha mapenzi ya wazi kwa Yanga ambao ni mahasimu wao wakubwa. Mashabiki wamesema kuwa toka mchezaji huyo amehama Yanga kwenda Azam hatajawahi kuifunga timu ya Yanga katika michezo ambayo wamekutana hivyo kuwa na mashaka kama anaweza kufanya hivyo akiwa na Simba. Kaburu amedai klabu hiyo imenunua mkataba wote aliokuwa nao Azam ambao ni wa mwaka mmoja kwa makubaliano maalumu ambayo hakutaka kuyaweka wazi.

No comments:

Post a Comment