Alex Song. |
KIUNGO nyota wa kimataifa wa Cameroon na klabu ya Arsenal anakaribia kusaini mkataba wa miaka mitano na klabu ya Barcelona ya Hispania. Kiungo huyo mkabaji ambaye ana umri wa miaka 24 amekubali kupewa mkataba huo ambao utamuwezesha kulipwa kiasi cha paundi milioni tano kwa mwaka na makubaliano hayo yamefanyika kabla ya klabu hiyo haijakutana na uongozi wa Arsenal kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho. Barcelona wameamua kumchukua song baada ya klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa kumnyakuwa mchezaji ambaye walikuwa wakimfukuzia kwa kipindi kirefu Thiago Silva kwa kumsajili kutoka klabu ya AC Milan kwa paundi milioni 42. Timu kwasasa inajipanga kurejesha taji lake la Ligi Kuu nchini Hispania ambalo walishindwa kulinyakuwa msimu uliopita na wanaamini kuwa Song ataimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo kutokana na kiwango bora kabisa alichokionyesha msimu uliopita. Msimu uliopita Song alitengeneza pasi za mwisho 11 ambazo zilizaa mabao ambayo yalifungwa na Robin van Persie na uwezo wake wa kucheza katika nafasi ya kiungo pamoja na kuzuia ndio vitu vilivyoivuta Barcelona kutoa hela ili kuhakikisha inapata saini yake. Kama mambo yakienda sawa Song atakuwa mchezaji wa pili wa Cameroon kucheza Barcelona baada ya Samuel Eto’o naye kukipiga katika klabu hiyo kwa mafanikio.
No comments:
Post a Comment