WAKONGWE wa soka nchini Misri timu ya Al Ahly itapambana na timu ya Sunshine Stars ya Nigeria katika nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika michuano hiyo mikubwa barani humu. Al Ahly walifanikiwa kuibuka vinara wa kundi B baada ya kufanikiwa kulazimisha sare ya bao 1-1 kwa mahasimu wao Zamalek katika mchezo uliochezwa jana jijini Alexandria. Kwa upande wa SunShine Stars wenyewe walifanikiwa kukata tiketi ya kucheza nusu fainali kufuatia kuenguliwa kwa timu ya Etoile du Sahel na Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kutokana na vurugu za mashabiki wa timu hiyo. Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini Nigeria inatarajiwa kuikaribisha Al Ahly katika nusu fainali ya kwanza ambayo inatarajiwa kupigwa kati ya Octoba 5,6 na 7 katika Uwanja wa Dipo Dina jijini Ijebu-Ode wakati nusu fainali ya pili itapigwa katika Uwanja wa Jeshi jijini Cairo kati ya Octoba 19,20 na 21. Mabingwa watetezi wa kombe hilo, timu ya Esperance ya Tunisia wao watapambana na TP Mazembe katika nusu fainali ya michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment