Thursday, September 13, 2012

CAMERON AWAOMBA WAFIWA WA TUKIO LA HILLSBOROUHG.

WAZIRI Mkuu wa Uingereza David Cameron amewaomba radhi watu waliopoteza ndugu zao na kueleza kama watu hao wamenyimwa haki mara mbili, kufuatia maafa yaliyotokea katika mji wa Hillsborough. Katika maafa hayo mashabiki wapatao 96 walikufa kufuatia taharuki uwanjani na kukanyagana tukio ambalo lilitokea katika Uwanja wa Sheffield mwaka 1989. Akizungumza baada ya kusoma ripoti huru ambayo ilifichua baadhi ya maelezo ambayo hayakuwa yamewekwa wazi hapo awali kufuatia mkasa huo, Cameron amesema maafisa wa polisi walishindwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu, na kisha kuwalaumu mashabiki wa klabu ya Liverpool. Trevor Hicks, ambaye ni kati ya watu ambao wamekuwa wakiongoza kampeni ya kufahamu ukweli, alisema ripoti hiyo inaonyesha kwamba maisha ya wengi yangeliweza kuokolewa kama huduma za dharura zingepatikana kwa haraka mara tu baada ya mashabiki kuanza kukanyagana. Bwana Hicks, ambaye binti zake wawili walifariki katika mkasa huo, alisema sasa wao watashinikiza hatua za kisheria kufuatia makosa ya kihalifu zichukuliwe katika kuhakikisha waliohusika wataadhibiwa.

No comments:

Post a Comment