Thursday, September 20, 2012

MAJERUHI YAIANDAMA BARCELONA.

MAJERUHI yameendelea kuiandama klabu ya Barcelona baada beki wake wa kati Gerard Pique naye kuumia katika mchezo wa jana ambapo anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili au tatu. Pique aliumia mguu wake wa kushoto wakati timu yake hiyo ikicheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Spartak Moscow mchezo ambao walishinda kwa mabao 3-2. Mara baada ya kuumia alipatiwa matibabu na kurejea tena uwanjani lakini muda mfupi baadae alishindwa kuendelea na nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji mpya aliyesajiliwa msimu huu akitokea Arsenal, Alex Song katika dakika ya 12 ya mchezo huo. Kuumia kwa mchezaji huyo kunaongeza orodha ya wachezaji majeruhi ambapo beki mwingine tegemeo wa klabu hiyo Carles Puyol na kiungo Andres Iniesta nayo bado wanauguza majeruhi walipata hivi karibuni. Pique anatarajiwa kukosa michezo miwili ya ligi ambapo Barcelona itaikaribisha Granada Jumamosi pamoja na ule wa ugenini dhidi ya Sevilla wiki moja baadae lakini anategemewa kuwemo katika kikosi kitakachopambana na Benfica Octoba 2 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

No comments:

Post a Comment