Thursday, September 27, 2012

MATOKEO YA CAPITAL ONE CUP.

TIMU ya Manchester United imefanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Ligi baada ya kufanikiwa kuifunga Newcastle United kwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Old Traford jana. Mbali na United mabingwa watetezi wa michuano hiyo Liverpool nao pia walifanikiwa kusonga baada ya kuifunga West Bromwich kwa mabao 2-1 mabao ambayo yalifungwa na mshambuliaji mpya aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka Real Madrid ya Hispania, Nuri Sahin. Katika michezo mingine ilishuhudia Tottenham Hotspurs ikiifunga Carlisle kwa mabao 3-0 huku mahasimu wao kutoka Kaskazini mwa jiji la London Arsenal wao wakifanya mauaji kwa kuibugiza Coventry City kwa mabao 6-1. Katika mchezo wa jana United walifanya mabadiliko ya wachezaji 11 ambao walicheza katika mchezo dhidi ya Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu Jumapili iliyopita huku mshambuliaji wake nyota Wayne Rooney akirejea baada ya kuumia goti wiki nne zilizopita pamoja na kiungo Darren Fletcher naye akirejea baada ya kuwa nje ya uwanja kwa miezi 10.

No comments:

Post a Comment