Friday, September 21, 2012

MEXICO KUGOMBANIA NAFASI YA KUANDAA KOMBE LA DUNIA MWAKA 2026.

Justino Compean.
OFISA mkuuu wa Shirikisho la Soka nchini Mexico, Justino Compean amesema kuwa nchi hiyo itaomba nafasi ya kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2026. Mexico imewahi kuandaa michuano hiyo mwaka 1970 na 1986 na kama wakifanikiwa kupata nafasi ya kuandaa michuano hiyo mwaka 2026 itakuwa nchi ya kwanza kuandaa michuano hiyo mikubwa kabisa duniani mara tatu. Compean amesema kuwa Mexico ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa wakati walipokuwa wenyeji wa michuano iliyopita hivyo wanahitaji tena kuandaa Kombe la Dunia lakini wanatarajia upinzani mkubwa kutoka Marekani. Brazil ambao ndio watakuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 watakuwa wakiandaa michuano hiyo kwa mara ya pili huku Urusi wenyewe watakuwa wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2018 na Qatar wataandaa michuano ya mwaka 2022. Nchi nyingine ambazo zimewahi kuandaa michuano hiyo mara mbili ni pamoja na Italia mwaka 1934 na 1990, Ufaransa mwaka 1938 na 1998 pamoja na Ujerumani mwaka 1974 kipindi hicho ikiitwa Ujerumani Magharibi na 2006.

No comments:

Post a Comment