Monday, September 24, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA KRFA, MARFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa vyama vya mpira wa miguu mikoa ya Kilimanjaro (KRFA) na Manyara (MARFA) katika uchaguzi uliofanyika juzi (Septemba 22 mwaka huu). Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KRFA na ule wa MARFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika mikoa hiyo. TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa kamati za utendaji za MARFA na KRFA zinazoongozwa na Elley Mbise na Goodluck Moshi, kwani viongozi hao wapya wana changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha wanaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba zao na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao. Pia tunatoa pongezi kwa kamati za uchaguzi za IRFA na MARFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF. 
Viongozi waliochaguliwa kuongoza MARFA ni Elley Mbise (Mwenyekiti), Wilson Ihucha (Makamu Mwenyekiti), Apollinary Kayungi (Katibu), Peter Abong’o (Mhazini), Khalid Mwinyi (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Phortinatus Kalewa (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Peter Yaghambe (Mjumbe). Kwa upande wa KRFA waliochanguliwa ni Goodluck Moshi (Mwenyekiti), Mohamed Musa (Katibu), Kenneth Mwenda (Mwakilishi wa Klabu TFF), Kusiaga Kiyata (Mhazini) na Denis Msemo (Mjumbe). Nafasi zilizowazi baada ya kukosa wagombea wenye sifa kwenye vyama hivyo zitajazwa baadaye.

WASHABIKI 65,458 WAZISHUHUDIA SIMBA, YANGA WIKIENDI
Mechi za Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara za Simba na Yanga zilizochezwa wikiendi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zimeshuhudiwa na washabiki 65,458. Yanga ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKT Ruvu, Jumamosi (Septemba 22 mwaka huu) mechi yao ilishuhudiwa na washabiki 15,770 wakati ile ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa jana (Septemba 23 mwaka huu) ilikuwa na washabiki 9,688. Simba ilishinda mabao 2-1. Wakati mechi ya Yanga iliingiza sh. 88,251,000 ile ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting Stars mapato yalikuwa sh. 55,454,000. Mechi ya Yanga kila timu ilipata sh. 19,846,194.92 huku ile ya Simba kila timu ilipata sh.11,350,774.58.

MECHI YA AZAM, MTIBWA SUGAR ZAINGIA MIL 2.5/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Azam na Mtibwa Sugar iliyochezwa juzi (Septemba 22 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi imeingiza sh. 2,509,000 ambapo kila timu imepata mgawo wa sh. 301,661. Washabiki 827 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Nayo mechi ya ligi hiyo kati ya African Lyon na Tanzania Prisons iliyochezwa jana (Septemba 23 mwaka huu) kwenye uwanja huo imeingiza sh. 245,000 huku kila timu ikipata sh. 32,286. Prisons ilishinda mechi hiyo kwa mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment