Monday, September 24, 2012

KLITSCHKO ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA SANDERS.

BONDIA nyota wa uzito wa juu Vitali Klitschko ametuma salamu zake za rambirambi kwa Corrie Sanders akimuelezea bondia huyo wa zamani wa uzito wa juu raia wa Afrika Kusini kama mpinzani mgumu zaidi kati ya wote aliopambana nao. Klitschko mwenye umri wa miaka 41 ambaye ni bingwa wa dunia wa uzito wa juu wa WBC alimuelezea Sanders kama bondia mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kushambulia na kukwepa masumbwi kipindi alichokuwa ulingoni. Sanders mwenye umri wa miaka 46 ambaye alifariki dunia Jumapili baada ya kupigwa risasi na majambazi waliovamia mgahawa aliokuwepo, alimpiga mdogo wake Vitali anayeitwa Wladimir katika pambano lililofanyika jijini Hanover, Ujerumani mwaka 2003. Alimsimamisha bondia huyo raia Ukraine ambaye kwasasa anashikilia mikanda ya ubingwa wa WBA, IBF, WBO na IBO katika raundi ya pili na kunyakuwa taji la WBO kipindi hicho. Sanders alipigana na Vitali katika pambano lililofanyika jijini Los Angeles, Marekani mwaka mmoja baadae kugombea mkanda wa WBC lakini alishindwa kuendeleza ubabe kwa ndugu hao na kudundwa katika raundi ya nane ya mchezo huo.

No comments:

Post a Comment