Friday, September 28, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

TFF YATOA ITC KWA WACHEZAJI WANNE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanne waliokuwa wakichezea timu mbalimbali nchini. Wachezaji hao ni Tony Ndolo aliyejiunga na KCC ya Uganda kutoka Toto Africans, Felix Amech Stanley aliyekwenda Bahla ya Oman kutoka Coastal Union, Ernest Boakye kutoka Yanga aliyejiunga na Tripoli Athletics Club ya Lebanon na Derrick Walulya aliyerejea URA ya Uganda kutoka Simba.

15 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI TWFA
Wanamichezo 15 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) utakaofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao. Waliochukua fomu za kuwania uenyekiti ni Lina Kessy, Isabellah Kapera na Joan Minja. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti imeombwa na Roseleen Kisiwa pekee wakati Katibu Mkuu ni Amina Karuma na Cecilia Makafu. Macky Mhango pia ni mwombaji pekee aliyeomba nafasi ya Katibu Msaidizi. Waombaji watatu wa nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni Furaha Francis, Juliet Mndeme na Zena Chande. Nafasi ya Mhazini nayo ina mwombaji mmoja tu ambaye ni Rose Msamila. Sophia Charles, Rahim Maguza, Telephonia Temba na Jasmin Badar Soud wao wanaomba nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho kwenye uchaguzi huo ambao utaendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya Ombeni Zavalla.

MKUTANO VODACOM, KLABU ZA LIGI KUU
Klabu za Ligi Kuu na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom zimekutana jana (Septemba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yalilenga kipengele ya upekee (exclusivity) kilichopo kwenye mkataba wa udhamini ambacho kitaendelea kuwepo. Klabu zilikuwa zimeomba kwa mdhamini kuangalia uwezekano wa kukiondoa. Pande hizo zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kuitafutia kila klabu mdhamini binafsi kwa lengo la kuhakikisha zinashiriki kikamilifu katika ligi hiyo. Klabu zote zimeshapata vifaa kutoka kwa Vodacom ukiondoa African Lyon ambayo ilitarajia kuchukua vifaa hivyo leo kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo.

MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VIONGOZI TAFCA
Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) unaanza rasmi Septemba 30 mwaka huu kwa uchukuaji fomu kwa wagombea. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, fomu kwa waombaji uongozi zitaanza kutolewa Septemba 30 mwaka huu, na mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ni Oktoba 4 mwaka huu. Fomu hizo zinapatikana ofisi za TAFCA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 alasiri. Ada ya fomu kwa waombaji wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi ni sh. 200,000. Nafasi zilizobaki za Mhazini, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ada ya fomu ni sh. 100,000. Uchaguzi wa TAFCA umepangwa kufanyika Novemba 10 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment