Tuesday, October 16, 2012

JAPAN YAKASIRISHWA NA UFARANSA.

JAPAN imeonyesha kukasirishwa na mtangazaji wa luninga ya French 2 ya nchini Ufaransa baada ya kuonyesha picha ya golikipa wa timu ya taifa ya Japan Eiji Kawashima akiwa na mikono minne na kutania kuwa imetokana na athari za kituo cha nyuklia kilicholipuka cha Fukushima. Akisifia kiwango alichokionyesha Kawashima katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa ambao japan ilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Ufaransa Ijumaa iliyopita mtangazaji huyo aitwaye Laurent Ruquier alitumia picha hiyo ambayo ilizua mtafaruku. Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Japan, Osamu Fujimura aliita kitendo cha Ruquier kutumia picha hiyo na kukumbushia tukio la kusikitisha la Fukushima lililotokea mwaka uliopita kwamba sio cha kiungwana. Aliongeza kuwa ubalozi wa Japan nchini Ufaransa wameshatuma barua kupinga tukio hilo lililorushwa na luninga ya France 2 kwani limewaumiza watu wahanga wa janga hilo ambao mpaka sasa wanajitahidi kuanza maisha mapya baada ya kupoteza ndugu na jamaa zao. Tetemeko la ardhi lenye kipimo cha magnitude 9.0 la chini ya bahari lililotokea Machi mwaka jana nchini humo na kusababisha tsunami liliua watu zaidi ya 15,000 na wengine 3,000 kuathirika kutokana na kituo cha nuklia cha Fukushima kulipuka kutoka na tsunami hilo.


No comments:

Post a Comment