Tuesday, October 2, 2012
NCHI TANO ZATUMA MAOMBI KUSHIRIKI CHALENJI.
NCHI tano wakiwemo mabingwa wa soka Afrika, Zambia zimetuma maombi ya kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji ambayo inaandaliwa na Baraza la Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA. Mbali ya Zambia nchi nyingine ambazo zimetuma maombi hayo ni pamoja na Cameroon, Malawi, Zimbabwe na Ivory Coast ambapo kwa mwaka huu michuano hiyo imepangwa kufanyika jijini Kampala, Uganda kuanzia Novemba 24 mpaka Desemba 8. Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alithibisha kutumwa kwa maombi hayo lakini amesema kuwa uamuzi utatolewa katika kikao cha bodi watakachokutana baada ya mechi za mzunguko wa mwisho wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2013. Katika michuano ya mwaka jana iliyofanyika jijini Dar es Salaam, nchi za Malawi na Zimbabwe ndio zilikuwa timu ngeni katika ukanda huu zilizopewa mwaliko na CECAFA. Musonye aliomba nchi wanachama wa CECAFA kuthibitisha ushiriki wao wa michuano hiyo mpaka ifikapo Octoba 8 ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya ratiba kamili kupangwa Novemba 8 mwaka huu jijini Kampala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment