BINGWA mtetezi wa Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika, Esperance ya Tunisia na Al Ahly ya Misri zinategemewa kukutana katika fainali ya michuano hiyo mara baada ya michezo yao ya nusu fainali mwishoni mwa wiki hii. Al Ahly ndio yenye rekodi nzuri ya kunyakuwa kombe hilo ikiwa imeshalichukua mara sita huku wakicheza fainali nane wakati Esperance wao wamechukua mara mbili na kumaliza katika nafasi ya pili mara tatu. Timu hizo mbili zinapewa nafasi ya kusonga mbele baada ya kulazimisha sare katika michezo yao ya nusu fainali ya kwanza waliyocheza ugenini ambapo Esperance ilifanikiwa kupata sare ya bila kufungana na TP Mazembe ya DRC wakati Al Ahly yenyewe ilitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Sunshine Stars ya Nigeria. Mchezo wa Al Ahly na Sunshine utachezwa katika uwanja mtupu baada ya tukio la kuuwawa kwa mashabiki 74 katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya mahasimu wao Al Masry Februari mwaka huu jijini Port Said. Mazembe wataifuata Esperance huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda ugenini kwa mabao 5-0 katika mchezo wa fainali ya kwanza kabla ya Esperance kuambulia sare ya bao 1-1 katika fainali ya pili na Mazembe kutawzwa mabingwa wapya wa michuano hiyo mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment